Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), pamoja na CRDB Foundation, imezindua mpango wa mikopo nafuu kwa wabunifu, ukihusisha Sh. Bilioni 4.6, ambapo serikali kupitia tume hiyo imetoa dhamana ya Sh. Bilioni 2.3.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda katika uzinduzi wa hafla hiyo amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha wabunifu hususan vijana, wanawezeshwa kwa vitendo ili kushiriki katika uchumi wa kisasa.
“Maelekezo ya Mheshimiwa Rais ni wazi kabisa: vijana wetu wabunifu wasaidie kujenga uchumi. COSTECH na CRDB Foundation wametekeleza agizo hilo kwa vitendo,” amesema.

Profesa Mkenda ameipongeza CRDB Foundation kwa kuonyesha mfano wa taasisi inayotambua fursa zilizopo kwa wabunifu wa Kitanzania, na kuitaka sekta binafsi na wadau wengine kuiga mfano huo kwa kuwekeza moja kwa moja katika miradi ya vijana.
“Kama kweli tunataka mapinduzi ya kiuchumi, basi tuwekeze kwenye akili na maarifa ya Watanzania,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema mchakato wa utoaji mikopo utaendeshwa kwa uwazi, kidigitali, na kwa kuzingatia usawa.
Amesema zaidi ya wabunifu 400 kutoka mikoa mbalimbali tayari wamepatiwa mafunzo na ushauri, wako katika hatua ya kuingia kwenye mfumo wa kupata mikopo.
“Hatutaki tena wazo zuri libaki mezani. Tunataka lionekane sokoni, lichangie pato la taifa, na lifungue ajira,”almesema.
Mpango huo pia unajumuisha vipengele vya mafunzo kabla na baada ya mkopo, ili kuhakikisha kuwa wabunifu wanatumia fedha walizopata kwa njia endelevu na zenye matokeo.
Mada kama akili bunifu, usimamizi wa biashara, na matumizi ya teknolojia ni sehemu ya kozi zitakazotolewa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, ameleza kuwa taasisi yao imejipanga kuhakikisha wabunifu wanaoungwa mkono wanapewa siyo tu fedha, bali pia mafunzo, ushauri, na mwongozo wa kitaalamu.
“Tunaamini kuwa ubunifu unaweza kuwa injini ya maendeleo ikiwa tu utapewa mazingira wezeshi ya kifedha na kiufundi,”amesema.