Kaimu Mkurugenzi Usuluhishi Awazungumzia
Na Lucy Ngowi
TUME ya Usuluhishi na Uamuzi ( CMA), inasaidia vijana kuwa na nafasi bora kazini, pia ina wajibu wa kutatua migogoro ya kikazi. .
Aidha utatuzi wa migogoro ya kikazi kwa vijana, itawasaidia kuendelea na uzalishaji kwa ajili ya kupata kipato.
Kaimu Mkurugenzi wa Usuluhishi CMA, Rodney Matalis amesema hayo alipokuwa akizungumza na Mfanyakazi kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Vijana.
Amesema CMA inajenga uelewa na utatuzi wa migogoro ya kikazi kwa vijana, kuwezesha ustawi wa vijana na taifa kwa kuwa watajikita katika uzalishaji mali.
Amesema katika kuwasaidia vijana ushirikiano kati ya vijana na waajiri unahitajika ili kuelewa mitazamo tofauti pamoja na kutafuta suluhu za kudumu.
“Vijana ni nguvu kazi kubwa katika kujenga uchumi hivyo tume ina wajibu wa kuhakikisha migogoro inayopelekwa na vijana inasikilizwa kwa njia ya usuluhishi kwa sababu,
” Inaharakisha utatuzi wa migogoro na kuwafanya vijana kujikita na shughuli za uzalishaji mali,” amesema.
Amesema katika kuhakikisha nguvu kazi hiyo inatumika kikamilifu ni wajibu wa tume hiyo kuwaelimisha vijana juu ya umuhimu wa usuluhishi,
Lengo likiwa ni kukuza uchumi kwa kuangalia kuwa kundi hilo ni kubwa hivyo likipata uelewa wa utatuzi wa migogoro ya kikazi kwa njia ya usuluhishi litafungua fursa mpya za ajira kwa sababu migogoro mingi itasuluhishwa na kuvutia uwekezaji.
“Pia kuwasaidia vijana kujifunza mbinu za usuluhishi wa migogoro ya kikazi kutawajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazoibuka mahala pa kazi,” amesema.