Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBUNGE wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Arusha, Chiku Athumani, amesema atahakikisha masuala ya afya na elimu yanapewa kipaumbele katika Bunge la 13, akisisitiza kuwa afya ya mama na mtoto ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii.
Amesema hayo nje ya viwanja vya Bunge jijini Dodoma katika Mkutano wa kwanza wa Bunge ka 13.
“Kama mama na mwakilishi wa wanawake, nitashirikiana na serikali kuhakikisha afya ya mama na mtoto inabaki kuwa kipaumbele cha kitaifa,” amesema Chiku.
Akizungumzia sekta ya elimu, Chiku amesema serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya shule, hatua iliyopunguza umbali wa wanafunzi kufika shuleni hadi wastani wa kilomita mbili pekee.
Aidha, amesema jukumu kuu la wabunge ni kuishauri na kuisimamia serikali, kuhakikisha kila mpango unaopitishwa bungeni unatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi.
“Kazi yetu si kupitisha bajeti pekee, bali kuhakikisha tunasimamia utekelezaji wake kwa uwajibikaji na uthubutu,” amesisitiza.
Chiku pia alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni mfano wa utekelezaji wa sera zenye matokeo chanya, ikiwemo kupungua kwa vifo vya akina mama na watoto wachanga kutoka 556 hadi 104 kati ya vizazi 100,000.

