Na Mwandishi Wetu
IDETE, MLIMBA: CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema kipo tayari kupambana na changamoto za maisha kwa Watanzania kwa kuhakikisha gharama za bidhaa muhimu zinapunguzwa ili wananchi waweze kumudu maisha yao ya kila siku.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Idete, wilayani Mlimba, Morogoro Mgombea wa Urais kupitia chama hicho, Salum Mwalim, amesema bei ya bidhaa kama sukari haipaswi kuwa juu ilhali viwanda vya kuzalisha bidhaa hizo vipo nchini.
“Haiwezekani mkoa wa Morogoro uwe na viwanda zaidi ya viwili vya sukari, halafu wananchi wanunue kilo ya sukari kwa Shilingi 3,000. Hali hii haikubaliki,” amesema.

Akizungumzia miundombinu, Mwalim amesema sera ya CHAUMMA inalenga kutengeneza barabara zote zilizo katika maeneo ya uzalishaji ili kusaidia wakulima na wananchi kwa ujumla kunufaika kiuchumi.
“Barabara ni msingi wa maendeleo. Tutahakikisha kila eneo la uzalishaji linafikika kwa urahisi ili kuongeza tija na kuinua maisha ya watu,” amesema.