Na Lucy Ngowi
BALOZI wa Tanzania nchini Comoro, Saidi Yakubu amesema wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa kwa usafiri majini kati ya Comoro na Tanzania wanapatwa na changamoto kubwa kwa sababu ya uelewa mdogo wa kanuni kwa watoa huduma wanaofanya shughuli hizo.
Balozi Yakubu, aliyasema hayo wakati alipokuwa akijadiliana na watumishi wa TASAC pamoja na wana diaspora waliopo katika Kliniki ya Diaspora katika viwanja vya Bunge la Comoro, mjini Moroni.
“Tulikaa na wadau wa TASAC ili kupata mrejesho, kwa kiasi kikubwa changamoto inayowakabili wafanyabiashara wa diaspora ni suala la uelewa wa huduma za meli, nani anapaswa kufanya nini, kwa mujibu wa sheria zinazoendesha usafiri majini,” amesema.
Amesema changamoto nyingine ambayo imebainika ni ukosefu wa uwepo wa vyombo imara na salama vya usafari majini vinavyotumika katika nchi ya Tanzania na Comoro,.
Katika hilo amesema juhudi mahsusi zinafanywa na upande wa Tanzania ili kuwa na vyombo kwa upande wa Tanzania ili kutatua changamoto hiyo.
“Suala lingine ambalo ni la kulifanyia kazi ni kuwa na vyombo imara vya usafiri utakaotumika katika nchi hizi mbili na kwa bahati nzuri tumeshapewa ahadi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwamba MV. Mapinduzi itakapopona itatumika kwa ajili ya usafiri kati ya Comoro na Tanzania,” amesema.
Hata hivyo, Yakubu amesema uwepo wa TASAC katika Kliniki hiyo umesaidia kutoa elimu kwa wadau wa usafirishaji na wafanyabiashara kwa ujumla kwa kuwa asilimia kubwa ya bidhaa za chakula zinazoingia Comoro zinatokea Tanzania kwa hiyo ni soko zuri na sekta ya usafirishaji ndio kiungo katika kuhakikisha bidhaa hizo zinafika Comoro.
Naye Ofisa Udhibiti Usafirishaji wa TASAC, John Butoto ametoa elimu kwa diaspora na kuwaasa kuhakikisha wanatumia watoa huduma wanaotambulika kisheria jambo ambalo litasaidia kufuatilia pindi wanapopata changamoto za kupotea kwa mzigo.
“Wafanyabiashara wengi mnashindwa kufikisha malalamiko yenu kwa mamlaka husika kwa sababu hamtumii watoa huduma sahihi,
“Orodha ya watoa huduma ambao wanatambulika kisheria ipo na tutaiwasilisha ubalozini kwetu ili muweze kuwatumia watoa huduma hao waliosajiliwa na kupewa leseni za kufanya huduma hizo na TASAC,” amesema