Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema miaka ya zamani vifo vya upasuaji vilikuwa vingi kutokana na kukosekana kwa utaalamu wa usingizi.
Chalamila amesema hayo wakati wa ziara ya Wilaya ya Ubungo, alipotembelea Kituo cha Afya Makurumla.
Amesema, ” Leo hii Rais Samia Suluhu Hassan amewekeza kupatikana kwa madaktari wa usingizi, madaktari wa Mama na mtoto na wale wa upasuaji,”.

Katika kituo hicho, Halmashauri ilitenga Sh. Milioni 350 kwa ajili ya Mradi wa Jengo la Watoto ambao ulianza mwaka 2023, ambapo mpaka sasa jengo la upasuaji limekamilika asilimia 100, na jengo la upasuaji asilimia 70.
Mradi huo ukikamilika utasaidia zaidi ya wananchi laki mbili kutoka Makurumla.
Wakati huo huo. Chalamila amepongeza Kanisa la Yesu la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa mchango mkubwa kwa Taifa katika kuboresha miundombinu ya Shule ya Msingi Msewe.

Amesema kanisa hilo limejenga madarasa 10, matundu manne ya vyoo pamoja na Ofisi ya Walimu.
