Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameagiza miradi kujengwa kwa viwango kulingana na thamani ya fedha, pia ikamilike kwa wakati uliowekwa.
Chalamila ametoa maagizo hayo alipofanya ziara ya kutembelea ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo Jimbo la Kibamba, Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam.

“Ni muhimu kufanya ujenzi wa miradi unaozingatia thamani ya fedha, miradi inayoweza kudumu kwa miaka mingi na ujenzi ukamilike kwa wakati ili kumaliza adha kwa akina mama na watoto ” amesema.
Pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa nyingi zinazowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo alupokuwa akiweka Jiwe la Msingi katika mradi wa jengo la mama na mtoto kwenye kituo cha afya cha Mpiji Magoe

Pia akiwa kwenye mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Goba Kulangwa Chalamila amesisitiza suala la ulinzi na usalama wakati nchi ikiwa inaelekea kwenye uchaguzi mkuu hivyo ameagiza kukamilishwa kwa ujenzi wa Kituo cha Polisi cha Tegeta A.
Naye Meya wa Manispaa ya Ubungo Juma Nyaigesha amewataka wananchi na wafanyabiashara kuto kukwepa kulipa kodi kwani ndio chanzo cha kupata fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo ikiwemo vituo vya afya.

Pia Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Mpiji Magoe Hereswida Cosmas akieleza maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo la mama na mtoto amesema ujenzi unaendelea vizuri na utakamilika kwa wakati.
Vile vile Chalamila ametembelea na kukagua mradi wa maji wa kibamba, pamoja na kukagua mradi wa shule ya sekondari Goba Kulangwa.

Katika ziara hiyo amemalizia kwa kufanya mkutano wa hadhara Kata ya Saranga eneo la ofisi ya Serikali ya Mtaa na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi ikiwemo ubovu wa barabara, changamoto ya TASAF, Maji, kusuasua kukamilika kwa ujenzi wa Zahanati ambapo ameahidi kabla ya kufika ijumaa ya wiki ijayo fedha zitakuwa zimepelekwa.
.