Na Lucy Ngowi
DODOMA: CHUO cha Usafiri wa Anga (CATC), kimeanzisha kozi inayohusisha wakulima ya urushaji wa ndege nyuki ambao kwa sasa ndio teknolojia inayotumika katika unyunyizaji wa dawa mashambani.
Ofisa Habari na Masoko Mkuu wa Chuo hicho, Ally Changwila amesema hayo wakati wa maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yajulikanayo kama nane nane, yanayofanyika Kitaifa jijini Dodoma.
‘Katika maonesho haya, Chuo cha Usafiri wa anga CATC, kimeamua kuleta kozi ambayo inahusika moja kwa moja na wakulima.
” Ni moja kati ya kozi nyingi zinazotolewa, ni lozi ya urubani wa ndege nyuki, ” amesema.
Maelezo yake ni kwamba, kozi hiyo inatolewa kwa wiki nne, wiki mbili darasani na wiki mbili kwa vitendo.
Amesema kozi hiyo inawapika watu namna ya kutumia ndege nyuki ambayo hutumika kumwagilia dawa kwenye mazao na kufanya ukaguzi ili kujua maeneo ambayo mazao yanavamiwa na wadudu ili baadaye kuyakinga.
Amesema kwa sasa mtu akirusha ndege nyuki bila kuwa na leseni inayotolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ataingia katika matatizo.