Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 6, 2026
Habari Lucy Ngowi 20

BRELA: Sajili Biashara Kulinda Jina, Fursa

Na Lucy Ngowi
GEITA: WAFANYABIASHARA na wajasiriamali wametakiwa kutumia fursa ya Maonesho ya Tisa ya Madini mkoani Geita kupata elimu na huduma za usajili wa biashara, kampuni, majina ya biashara na nembo ili kulinda shughuli zao na kuongeza fursa za kibiashara.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Ofisa wa wakala huo, Salum Makuka, amesema huduma hizo zimefikishwa kwenye maonesho hayo ili kuwawezesha wananchi kupata elimu na huduma za usajili kwa urahisi.
Habari Picha 13837
Amesema huduma zinazotolewa ni pamoja na usajili wa kampuni, majina ya biashara, nembo za biashara, viwanda vidogo, leseni za biashara za Daraja A pamoja na usajili na ulinzi wa bunifu kupitia hati miliki.
Makuka amesema wananchi wanaofika katika banda hilo hawatozwi gharama ya kurahisishiwa huduma, bali hulipa ada rasmi ya Serikali kulingana na huduma wanayoomba.
Amesema usajili wa biashara ni muhimu kwa kuwa benki na taasisi nyingine za fedha huhitaji nyaraka halali za biashara wakati mfanyabiashara anapotaka kupata mkopo au kushiriki zabuni.
Ameonya kuwa kutosajili jina la biashara kunaweza kusababisha mfanyabiashara kupoteza haki ya kulitumia iwapo mtu mwingine atalitangulia kulisajili.
“Unaweza kuanzisha biashara kwa juhudi kubwa, lakini mtu mwingine akaja na kusajili jina hilo,” amesema.
Makuka pia amewataka wananchi kutumia mfumo wa BRELA wa BOS kujifunza namna ya kusajili biashara mtandaoni, kuwasilisha taarifa za mwaka na kulipia ada za uendelezaji wa majina ya biashara.
BRELA itaendelea kutoa huduma kwenye maonesho hayo hadi Septemba 3.
Habari Picha 13838
Naye mfanyabiashara wa Nayubi Cosmetics, amesema amepata uelewa mkubwa kuhusu umuhimu wa usajili wa biashara na nembo baada ya kupata elimu kutoka kwa maofisa wa BRELA katika maonesho hayo.

Amesema mwaka uliopita alifanikiwa kusajili jina la biashara kupitia BRELA, lakini hakuwa akifahamu umuhimu wa kusajili nembo ya biashara hadi alipofika kwenye maonesho ya mwaka huu na kupata elimu zaidi.

Amesema baada ya kupata elimu hiyo, alisaidiwa kukamilisha taratibu za usajili zinazohusiana na biashara yake, hatua aliyosema imemsaidia kuelewa mahitaji ya kisheria na namna ya kulinda jina na utambulisho wa biashara.

Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.