Na Mwandishi Wetu
TAASISI isiyo ya kiserikali ya BRAC Tanzania, imesema upo umuhimu kwa wadau mbalimbali kutoka sekta binafsi, kushirikiana na serikali na watunga sera kupunguza umasikini kwenye jamii nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Joydeep Roy wakati wa kusherehekea miaka 53 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo.
Amesema BRAC ni miongoni mwa taasisi zisizo za serikali ambazo zimekuwa zikitenga sehemu ya mapato yake, kurejesha kwa jamii hususani katika mambo yanayowagusa wananchi moja kwa moja,

Ikiwamo katika aneo la makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya watoto wadogo, uwezeshaji wa vijana, sekta ya elimu, kilimo, programu ya kuondoa umasikini.
“Na tunafanya hivyo kama sehemu ya kurudisha shukrani kwa jamii na kuiunga mkono serikali katika kuhudumia jamii ya Watanzania.
“Kwa mfano katika kusherehekea miaka 53 tangu kuanzishwa kwa taasisi yetu, mwaka huu tumejumuika na jamii kwa kutoa vifaa muhimu kwenye sekta ya elimu katika shule ya wasichana ya kulea watoto yatima ya Bethesaida iliyopo Mbezi Mpiji Magohe,”amesema.
Joydeep amesema taasisi yao itaendelea kujitolea kusaidia makundi mbalimbali ili kuhakikisha inakuwa sehemu ya kuongeza thamani kwenye maisha ya Watanzania.
“Mwaka huu tumekusudia kuongeza jitihada zaidi katika kuwa karibu na jamii katika kukuza umoja na ushirikiano na tumepanga kuwa na mijadala mbalimbali ya kujenga,
” Tunaamini mijadala hiyo itatoa fursa ya watu kusema changamoto, uvumbuzi pamoja na mambo hasi na chanya wanayokutana nayo,” amesema.
“Bado tunaamini kwamba tutaendelea kuongeza miradi mingine kwa ajili ya kusaidia jamii yetu kwa sababu sisi sote tunapaswa kuwajibika kuihudumia na si serikali pekee,” amesema.
Mwenyekiti na mwanzilishi wa Shule ya Sekondari Bethsadia , Raymond Machary pamoja na kuishukuru BRAC kwa msaada kwao, amesema bado shule hiyo ina uhitaji wa misaada kwa kuwa inachukua wanafunzi wenye uhitaji ambao wengi wao hawana wazazi.