Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM:”BABA Askofu Severine Niwemugizi, nataka nikupongeze sana kwanza kwa kuwaza mambo makubwa, na kutokuwaza vitu vidogo,””.
Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko, ambaye amemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, amesema hayo wakati wa Harambee ya Ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Rulenge- Ngara mkoani Kagera, ambalo ili likamilike zinahitajika Sh. Bilioni 7.7.

Katika harambee hiyo zimepatikana Sh. Bilioni 2.164 zikiwemo fedha taslimu na ahadi.
Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati amesema, ,” Tuna bahati mbaya watu wengi tunawaza vidogo, tukipata kidogo tunalalamika na Baba Askofu amewaza kikubwa ili apate kikubwa aridhike,”.
Amesema pamoja na kwamba Rulenge ni pembezoni, linaweza kufanyika jambo kubwa sawa na linaloweza kufanyika Dar es Salaam.

Amesema alichojifunza kwa Askofu Niwemugizi ni kwamba kila jambo ni mipango, na yeyote aliyepanga vizuri atafanikiwa, ambaye hakujipanga atabakia kuwa mlalamishi.
Amesema amemtafsiri Askofu huyo kwamba anatamani wakati wote jambo zuri litokee kwa watu wake, pia ni mbeba maono anachokihitaji ni kuungwa mkono.
Awali Biteko amesema Rais Samia alimwagiza amsaidie Askofu Niwemugizi ili jambo hilo lifanikiwe.

Kwa upande wake Askofu Niwemugizi amemshukuru Rais Samia kwa kumtuma Dkt. Biteko kusimamia harambee hiyo.
Amesema hivi sasa kanisa lililopo lililoanzishwa mwaka 1960 siyo imara kwa kuwa limechoshwa na nyundo za upanuzi na ukarabati, hiyo ndiyo sababu imewasukuma kujenga kanisa jipya.