DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri Wa Nishati, Dotto Biteko amesema kama kuna mahali panapaswa kuwekezwa mkazo zaidi ni kwenye ufundi stadi.
Biteko amesema hayo wakati akifunga Maadhimisho ya Miaka 30 ya Uanzishwaji wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), yaliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Dar es Salaam (JNICC).
Akifafanua hilo amesema, tafiti zinaonyesha ikiwekezwa dola moja kwenye ufundi stadi, kitakachopatikana ni sawa na kupata dola nne.
“Bahati njema tunapomfundisha mtoto tunamfundisha kwenye nyanja tatu za ujifunzaji. Tunamfundisha kwenye nyanja ya utambuzi, nyanja ya uelekeo pamoja na ustadi,” amesema.
Amesema katika miaka ya karibuni imekuwa ni kawaida kuona mtoto amemaliza kidato cha sita kwa mfano au ana digrii ya kitu Fulani lakini hawezi hata kujipikia chakula mwenyewe au kujifulia.
“Hakuna taifa lolote linaendelea bila kuwekeza watu kwenye stadi Fulani. VETA wakati inaendelea yapo matishio yanayotishia stadi mbalimbali. Tunafundisha watoto wetu na mabadiliko ya tabia ya teknolojia duniani yamekuwa tishio kubwa sana,” amesema.
Pia amesema kwa miongo miwili sasa sekta ya uzalishaji ilishuka kwa asilimia 20 na sekta ya huduma ikapanda kwa asilimia 27, ni kwa sababu ya uwepo wa mitambo ambayo inafanywa na watu wengi zaidi.
Amesisitiza kuwa wakati wanafundisha vijana wanawafundisha kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazokuja.
Vile vile amesema kuwa maadhimisho hayo ya VETA yamefanikiwa kwani uongozi na watumishi wake wameifanya iweze kufurukuta kila mmoja aizungumze kwa mtazamo anaouona.