Na Lucy Ngowi
DODOMA: JESHI la Magereza limetakiwa kusimamia kikamilifu mpango wa kuwapa ujuzi na mafunzo ya ufundi stadi wafungwa wanapokuwa gerezani.
Aidha wafungwa hao watakaohitimu mafunzo watatunukiwa vyeti vinavyotambuliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA), wanapomaliza vifungo vyao ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea wanaporudi katika jamii.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innnocent Bashungwa ameeleza hayo alipofanya ziara ya kikazi Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Dodoma.

Bashungwa amesema Jeshi hilo kwa kushirikiana na VETA litaanza utekelezaji wa mpango wa kuwapa mafunzo Wafungwa wanapokuwa gerezani.
Amesema mpango huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais, Samia Suluhu Hassan kwa Jeshi la hilo.
“Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, kuwapa ujuzi kwa kuwaendeleza wanaoingia gerezani na ujuzi,
“Lakini wale wanaoingia hawana ujuzi kabisa, kuangalia namna ya kuwapa ujuzi ili wanapotokaa waweze kujikimu kimaisha,” amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa, amemshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuliboresha Jjeshi hilo kwa kulipatia vifaa na vitendea kazi, pamoja na mabasi saba ya kusafirisha maabusu ambayo ameyazindua.
Bashungwa baada ya kuzindua mabasi hayo, amemtaka Kamishna Jenerali wa Magereza Jeremiah Katungu na menejimenti kusimamia na kutunza mabasi hayo.
Naye Kamishna Jenerali wa Magereza Jeremiah Katungu ameishukuru Serikali kwa kuliwezesha jeshi hilo. kununua magari mapya ikiwa pamoja ya mabasi ya kusafirisha mahabusu kutoka gerezani kwenda mahakamani ili kuwasaidia watuhumiwa kesi zao kusikilizwa na haki kutendeka kwa wakati.