Na Lucy Ngowi
DODOMA: BARAZA la Uuguzi na Ukunga Tanzania, limesema endapo mgonjwa atakuwa hajaridhika baada ya kufikisha malalamiko yake katika Kituo cha Afya hadi mkoa, basi afike katika baraza hilo.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa baraza hilo, Ndimnyake Mwakapiso amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea jijini Dodoma.
Amesema, “Kwa wenye malalamiko kama kuna mgonjwa hakutendewa sawasawa kuna ngazi ya malalamiko kuanzia kituo cha afya hadi mkoa na kama hajaridhika anaweza kwenda Baraza la Ukunga na uuguzi kupeleka malalamiko,”.
Amesema mara nyingi kupitia maonesho mbalimbali wamekuwa wakielimisha wananchi kupitia njia mbalimbali ili wananchi wajue baraza hilo ni chombo chao cha kufikishia kero wanapokuwa na shida.
Amesema baraza hilo linasimamia taaluma ya uuguzi na ukunga kuhakikisha kundi hilo kubwa la watoa huduma kwa kufuata misingi, taratibu, miiko, kanuni na sheria.
“Yapo majukumu mengi ambayo baraza linafanya, moja kati ya majukumu makuu ni kumshauri waziri wa Afya kuruhusu masuala yote ya sera ya uuguzi na ukunga, kama kuna marekebisho, kuna kitu cha kuongeza,” amesema.
Amesema baraza hilo ni muhimu kwa kuwa chuo hakiwezi kutoa taaluma ya uuguzi au ukunga bila kusajiliwa na baraza hilo.
Katika hatua nyingine, amesema mwaka jana wa fedha kulikuwa na mashauri takribani 26 ambayo waliyapokea, hivyo wapo wahusika waliopewa onyo na wengine kusimamishwa kazi miaka miwili.