Na Danson Kaijage.
ASKOFU wa Kanisa la Baptisti Jimbo la Kati, Anthony Mlyashimba amekemea mmomonyoko wa maadili unaofanywa na wafanyabiashara wanaotumia midoli yenye maumbile ya kike kuivalisha nguo za ndani, kuifunga shanga kisha kuiweka hadharani.
Mlyashimba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Madhehebu katika Mkoa wa Dodoma, amesema wafanyabiashara wengi wa nguo za kike wamekuwa wakifanya hivyo sio kuchangia mmonyoko wa maadili lakini pia inadhalilisha utu wa mwanamke au mwanaume.
Ameshauri serikali kupitia wizara zake zinazohusika iangalie namna nzuri ya wafanyabiashara kuweka biashara zao lakini siyo kutumia hiyo midoli.
“Kwa hivi sasa ni aibu kutembea na mtoto ,mama Mkwe au baba mkwe kupitia kwenye maduka ya nguo kutokana na midoli ambayo imevalishwa nguo za aibu hususani za nguo za ndani.
“Kutokana na hali hiyo Serikali inatakiwa kuona namna ya kupambana na hali hiyo ili kuendeleza maadili ya kitanzani badala ya kuyabomoa kwa kupitia mambo ambayo yanaonekana kama ni ya kawaida,” amesema.
Pia amewataka wazazi na walezi kukaa karibu na watoto wao kwa nia ya kuzungumza nao na kujua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ili waweze kuwajenga kimaadili.