Na Lucy Ngowi
DODOMA: ASKARI wawili wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wamefariki, na wengine wanne kujeruhiwa katika mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo ( DRC) yaliyofanywa na waasi wa M23 Januari 24 na 28, mwaka huu 2025.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiamo JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda amesema hayo katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari.
Kanali Ilonda amesema majeruhi hao wanne wanaendelea kupatiwa matibabu mjini Goma,
“Taratibu za kusafirisha miili ya marehemu wetu pamoja na majeruhi waliotokana na mapigano hayo zinaendelea kupitia Sekretareti ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrka (SADC), Mwenyezi Mungu awake uponyaji wa haraka majeruhi wetu,” imesema taarifa hiyo.
Amesema vikundi vya JWTZ vilivyoko nchini DRC, vipo salama, imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya uongozi wa SADC.
Amesema JWTZ limekuwa likishiriki shughuli za ulinzi wa amani chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya za Kikanda ikiwemo SADC.
“JWTZ limeshiriki kulinda amani katika nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Lebanon, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Liberia, Msumbiji pamoja Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( DRC),” amesema.
Pia JWTZ linaendelea kulinda amani kwa mwamvuli wa Jumuiya ya Naendeleo Kusini mwa Afrika huko Mashariki mwa nchi ya DRC, eneo ambalo limekumbwa na mgogoro uliozua mashambulizi kati ya waasi wa M23, wanaopambaba na jeshi la DRC katika maeneo hayo.