Na Danson Kaijage
DODOMA:Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka ameshauri kukata bima ya afya kwa ajili ya usalama wa afya kwani asilimia 22 ya vijana wanakabiliwa na magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza.
Dkt. Isaka amesema hayo wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari wenye lengo la kuelezea utekelezaji wa maendeleo kwa kipindi cha miaka minne inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema utafiti uliofanywa kwa kipindi cha mwaka 2021/22 umeonyesha kuwa asilimia hiyo ya vijana wana tatizo hilo ikiwemo afya ya akili.
Kutokana na hali hiyo watanzania wote wametakiwa kukata bima ya afya ya NHIF wakati wakiwa na afya badala ya kusubiri waanze kupata tatizo la kiafya jambo ambalo haliwezi kuwasaidia kwa ufasaha kama ambavyo wangekata bima wakati wakiwa na afya njema.
Akizungumzia zaidi juu ya mafanikio kwa kipindi hicho, amesema mfuko huo umefanikiwa kuimarisha mifumo ya TEHAMA inayorahisisha utendaji wenye tija.
Amesema kuwa madai ya watoa huduma za afya yanafanyika ndani ya siku 60 ikilinganishwa na siku 120 za awali kabla ya uwepo wa mifumo
Pia amesema katika kipindi hiki cha miaka minne wamesajili wamesajili wanachama milioni 2.2
Kuhusu ukusanyaji wa michango amesema umefikia Sh. Trilioni 2.3 kwa sasa kutokana na maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita.
Amesema Sh.Trilioni 2.29 zimelipwa kwa watoa huduma waliohudumia wanachama wa NHIF, na Sh. Bilioni 91 zimelipwa kwa watoa huduma waliohudumia wanachama wa NHIF ambao ni wastaafu.
Vile vile amesema wamefanikiwa kuokoa sh Bilioni 22 kutokana na usimamizi madhubuti wa mfuko wa NHIF, fedha hiyo ilikuwa inapotea kutokana na udanganyifu wa baadhi ya wanachama
Pia amesema tayari watumishi 36 wa vituo vya kutolea huduma wamechukuliwa hatua kwa kufanya udanganyifu kwenye mfuko.
Katika mafanikio hayo amesema kuwa Mfuko una ziada ya Sh. Bilioni 95 kwa sasa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma ambapo ulikuwa na nakisi.