Na Mwandishi Wetu
NAIROBI KENYA: Shirika la kimataifa la Article 19 Afrika Mashariki limeahidi kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) kuwajengea uwezo wanahabari katika masuala ya sheria za habari, haki za wanahabari na kupinga ukatili dhidi ya waandishi wanawake.
Makubaliano hayo yalifikiwa jijini Nairobi baada ya mkutano wa taasisi za habari kutoka nchi za Afrika Mashariki uliolenga kujadili uhuru wa vyombo vya habari na ushirikiano wa kikanda.

Naibu Mkurugenzi wa Article 19, Patrick Mutahi, amesema taasisi hiyo inatambua changamoto zinazokabili sekta ya habari na itashirikiana na JOWUTA kutekeleza miradi ya kusaidia wanahabari kupitia ufadhili wa wadau kama Jumuiya ya Madola.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Mussa Juma, amesema chama hicho chenye wanachama zaidi ya 400 kinahitaji ushirikiano huo ili kuboresha mazingira ya kazi, kukuza uwezo wa kiuchumi wa wanahabari na kuimarisha majadiliano na waajiri.
Naye Mkurugenzi wa Programu wa Chama cha Waandishi wa Kujitegemea Kenya (KCA), William Oloo-Janak, amesema changamoto za sekta ya habari Afrika Mashariki zinafanana, hivyo ushirikiano wa kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni muhimu.

Vyama vya wanahabari kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda vilikubaliana kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kutetea sera na sheria bora za habari pamoja na kupinga ukatili dhidi ya wanahabari wanawake.
