Na Danson Kaijage
MGOMBEA Ubunge kupitia Jimbo la Dodoma Mjini, Robert Mwinje amesema atajitahidi kupambana na changamoto ya ajira kwa vijana endapo atachaguliwa kuwa mbunge.
Aidha ameahidi kutafuta fursa za ajira rasmi na zisizo rasmi kwa vijana ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Mwinje amesema hayo wakati akijinadi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Kata ya Nala, baada ya kuulizwa na mmoja wa wajumbe, Maiko Majoya, kuhusu mikakati yake ya kusaidia vijana kupata ajira.

Katika mjadala huo, pia ametakiwa kufafanua namna atakavyoshughulikia migogoro ya ardhi, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakidhulumiwa kutokana na kutokuwa na hati miliki.
Akijibu maswali hayo, Mwinje ameeleza kuwa endapo atapata ridhaa ya wananchi, atahakikisha anasimamia kikamilifu maslahi ya vijana na kuhimiza upangaji wa ardhi pamoja na utoaji wa hati miliki kwa wananchi wote ili kuzuia migogoro isiyo ya lazima.
Kwa upande mwingine mgombea ubunge Fatuma Waziri akijinadi mbele ya wajumbe wa mkutano huo, amesema iwapo atapewa nafasi hiyo, atajikita zaidi katika kuboresha huduma za afya, hususan kwa wazee na watu wenye mahitaji maalum.
Kuhusu elimu, Waziri ameeleza anatambua juhudi za serikali kupitia sera ya elimu bure, lakini changamoto bado zipo.
Amesema ni muhimu kuendelea na mijadala ya wazi na wananchi ili kuibua njia bora zaidi za kuboresha sekta ya elimu nchini.