Na Lucy Ngowi
MBEYA: MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore, amesema VETA imejipanga kuhakikisha Watanzania wanapata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira la kisasa kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Akizungumza alipotembelea Chuo cha VETA Mkoa wa Mbeya, Kasore amesema taasisi hiyo inaendelea kuboresha karakana na vifaa vya kufundishia ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia, hususan katika fani kama umeme wa magari, useremala, ushonaji wa mabomba, urembo na ususi.
“Dunia ya leo inahitaji mafundi wanaotumia teknolojia kugundua matatizo, si kusikiliza sauti ya gari. Mafunzo yetu sasa yanazingatia hilo,” amesema.
Kasore ametaja pia kuwa VETA imeanza kutoa mafunzo ya sanaa za maonyesho kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na Bodi ya Filamu, ili kukuza vipaji katika uandaaji wa video, muziki na tamthilia.
“Ujuzi si lazima uwe kiwandani. Hata sanaa ni eneo la ajira na kipato, na VETA tunalipa uzito huo,” amesema.
Kwa upande wa watu wenye mahitaji maalum na wanaoishi mazingira magumu, Kasore amesema VETA hutoa mafunzo kwa zaidi ya watu 1,000 kila mwaka kupitia miradi maalum na ina miundombinu rafiki kwa makundi hayo.
Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa vyuo vipya 65 unaoendelea nchini kote ni sehemu ya mpango wa serikali kufikisha elimu ya ufundi karibu zaidi na wananchi, kwa kuzingatia mahitaji ya kiuchumi ya kila eneo.
Kasore pia amebainisha kuwa Oktoba 17, VETA itakutana na waajiri na wadau wa viwanda kwa lengo la kuboresha mitaala na kuimarisha ubora wa mafunzo.
“Ushirikiano na waajiri unahakikisha tunazalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika kazini,” alisema.
Kwa ujumla, Kasore amesisitiza kuwa dhamira ya VETA ni kumwezesha kila Mtanzania kupata ujuzi utakaomsaidia kuajiriwa, kujiajiri au kuajiri wengine – ikiwa ni mchango muhimu kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.