Na Lucy Ngowi
GEITA: BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wachimbaji wa madini, hususan wa dhahabu, kujiunga katika mfumo rasmi wa kifedha kwa kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu ili kusaidia kukuza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa taifa.
Meneja wa Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BOT, Victoria Msina, amesema hayo alipokuwa akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko alipotembelea banda la benki hiyo katika Maonesho ya Nane ya Madini yanayomalizika leo, Septemba 28, 2025.
Msina amesema BoT kwa sasa imejikita katika kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati, na kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi ya mifumo ya kifedha, ikiwemo uwekezaji katika dhamana za serikali.
Amesema Elimu hiyo inatolewa katika vituo mbalimbali vya BoT nchini pamoja na kwenye maonyesho na mikutano ya sekta ya madini.
Pia amesema katika maonesho hayo wachimbaji mbalimbali wamejitokeza katika banda la BOT kupata ufadanuzi mbalimbali.
“Tunawasihi waje tuwafundishe kwa sababu wakielewa mfumo huu, wataweza kujiinua kiuchumi na kuiwezesha serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia uwekezaji wao kwenye dhamana,” amesema.
Ameongeza kwamba BoT inatoa elimu ya fedha kwa wachimbaji juu ya namna bora ya kukopa kwa malengo, matumizi sahihi ya fedha, pamoja na kutumia mifumo rasmi ya malipo inayosimamiwa na BoT. “Unakopa kwa malengo, si kwa kununua vitu visivyo na maendeleo,” amesema.
Benki Kuu ya Tanzania inatarajia kupitia ushirikiano huo, wachimbaji wa madini watachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa taifa na kukuza ustawi wao binafsi kupitia maarifa ya kifedha.