Na Mwandishi Wetu
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia CCM, Dkt. Doto Biteko, amewapongeza wananchi wa Kata ya Bugelenga kwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo barabara, shule na maji.
Ametoa pongezi hizo jatika kampeni ambako ameeleza Serikali imepeleka umeme katika vijiji vyote vya kata hiyo, na sasa wanakamilisha kupeleka umeme vitongojini.

Dkt. Biteko ameahidi kuwa wananchi watakaounganishiwa umeme watapewa majiko ya umeme bure ili kupunguza gharama za kupikia.
Aidha, amesema CCM ikipewa tena ridhaa, watajenga kituo cha kupoozea umeme kitakachohudumia hadi Mbogwe, pamoja na kuongeza madarasa, maabara na jengo la utawala.
Amesisitiza kuwa shule zinazohitaji ukarabati zitashughulikiwa, na wodi ya kulaza wagonjwa itajengwa Bugelenga. Pia, amewaasa wananchi kuendelea kuwasomesha watoto wao, akibainisha kuwa Serikali inalipa ada hadi kidato cha sita.

Mgombea huyo pia amewasihi wananchi kumpigia kura mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa ametekeleza miradi mingi ya maendeleo katika eneo hilo. Ameeleza kuwa kipindi kijacho kitaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi kama maji, shule na afya.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa kata hiyo, Donald Rubigisa, amemshukuru Dkt. Biteko kwa kusaidia daraja kubwa na kuahidi kuendelea kushirikiana na wananchi kutatua changamoto kama ukarabati wa shule, uhaba wa chumba cha kuhifadhia maiti na mawasiliano duni ya simu.