Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: “NINAMSHUKURU Mungu kwa neema katika nafasi hii aliyonipatia. Udaktari huu nilioupata unaonyesha kwamba ahadi za Mungu katika maandiko ni za milele, zinaendelea kuishi, zinafundisha utumishi wetu ukikubalika katika jamii, inakutambua hata kama huna fedha.”
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Dkt. Suleiman Ikomba amesema maneno hayo baada ya kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu katika Utawala na Maendeleo ya Rasilimali Watu, na Chuo cha In His Name Bible College (IHNBC) cha nchini Marekani

Dkt. Ikomba amesema safari ya mwanadamu aijuaye ni Mungu peke yake, hivyo heshima aliyoipata imempa chachu ya kuendelea kulitumikia taifa na jamii ya Tanzania kwa nguvu na ari ya juu.
“Heshima hii inaniondoa katika aina nyingine yoyote ya ujinga-ujinga. Inanifanya kila jicho liniangalie. Tumaini langu ni kuwasaidia wengine kufikia matarajio yao,” amesema.

Amesema kwa nafasi yake ndani ya CWT, amepewa mzigo kwa lazima kusaidia taifa lake. Heshima ambayo inampa chachu ya kuendelea kuitumikia jamii ya Tanzania kwa nguvu, ikiwa ni pamoja na kutatua migogoro na kupooza mioyo ya watu iliyoumia, ili awe sababu ya kuwa faida kwao na kwa Chama cha Walimu.
“Sasa maana yake ni kuweza kuunganisha. Nimepewa mzigo kuhakikisha kwamba lazima nisaidie taifa langu nikiwaunganisha walimu katika mafanikio yao na katika hali ya kusimamia mambo mbalimbali wanayoyapata kwa hekima.” Amesema.
IHNBC kimemtunuku Ikomba kwa kutambua mchango wake mkubwa katika uongozi na maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Hafla hiyo ya mahafali ya pili ya chuo hicho imefanyika Septemba 13, 2025 jijini Dar es Salaam, katika Kanisa la Baptist, Kinondoni B, ambapo jumla ya wahitimu 21 walitunukiwa vyeti vyao katika ngazi mbalimbali za kitaaluma.