Na Mwandishi Wetu
BARAZA la Mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) limehitimisha Kikao chake cha Kawaida jijini Antananarivo, Madagascar, Agosti 14, mwaka huu 2025.
Kikao hicho ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC.

Ujumbe wa Tanzania uliwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Katika kikao hicho, Madagascar ilipokea rasmi Uenyekiti wa SADC kutoka Zimbabwe. Mawaziri walijadili ajenda mbalimbali zenye lengo la kuimarisha ushirikiano na mtangamano wa kikanda, ambao umetajwa kuwa njia muhimu ya kufanikisha maendeleo endelevu kwa nchi wanachama.

Miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa ni pamoja na hali ya michango ya nchi wanachama na taarifa ya utekelezaji kutoka kwa Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, kuhusu masuala ya uchumi, siasa, amani na usalama;
Pia utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Mawaziri pamoja na maamuzi ya Wakuu wa Nchi na Serikali; hali ya kuridhiwa kwa itifaki na nyenzo nyingine za kisheria za SADC; pamoja na ajenda zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Mikutano ya SADC itaendelea Agosti 15, 2025 kwa Mkutano wa Utatu wa Makatibu Wakuu na Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama, na kufuatiwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Asasi hiyo Agosti 16, mwaka huu 2025.

Tanzania inashikilia Uenyekiti wa mikutano hiyo ya Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama.
