Na Danson Kaijage
DODOMA: MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, wanatarajiwa kufika katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi kesho Agosti tisa, 2025 saa 4:50 asubuhi kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ratiba rasmi ya Tume ya Uchaguzi, ambayo imepanga uchukuaji wa fomu za urais kufanyika kuanzia Agosti tisa hadi 27, mwaka huu 2025.
“Chama chetu kilishakamilisha mchakato wa ndani na kuwateua wagombea. Hivyo, kesho watachukua fomu rasmi na baadaye kurejea makao makuu ya chama kwa ajili ya kusaini na kuzungumza na wanachama,” amesema.
Aidha, alibainisha kuwa uchukuaji wa fomu za ubunge na udiwani utaanza rasmi Agosti 14 na kufungwa Agosti 27, 2025 saa 10:00 jioni, sambamba na fomu za urais.
Makalla amesisitiza kuwa siku ya kuchukua fomu ni ya kihistoria kwa CCM, na kwamba chama kimejipanga kuhakikisha kinaendelea kushika dola kwa kipindi kingine.