Na Lucy Ngowi
MOROGORO: MBALI na miwa, TARI Kibaha inahusika pia na uzalishaji wa mbegu bora za muhogo na viazi vitamu.

Mtafiti kutoka TARI Kibaha, Msajigwa Mwakyusa, amesema hayo katika maonesho ya nanenane Kanda ya Mashariki yanayoendelea mkoani Morogoro.
Amesema taasisi hiyo ina aina 25 za mbegu bora za muhogo ambazo zinastahimili ukame, zina tija ya zaidi ya tani 20 kwa hekta pia zina ukinzani dhidi ya magonjwa ya batobato na michirizi ya kahawia
Amesema mfumo rasmi wa upatikanaji wa mbegu umewekwa ambapo TARI huzalisha mbegu za awali, kisha wadau wengine huzalisha daraja la msingi, cheti na umbegu.

“Aina ya Kiroba hukomaa kati ya miezi nane hadi 12, na huweza kutoa mavuno ya hadi tani 31 kwa hekta,” amesema.
Kwa upande wa mbegu za viazi vitamu amesema TARI Kibaha ina aina 20 za viazi vitamu, ambapo mbegu 12 kati yake ni viazi lishe.
“Mbegu hizi zinatoa tija ya zaidi ya tani 10 kwa hekta, zinakomaa ndani ya miezi minne, zinastahimili ukame na magonjwa ya virusi pamoja na zinakabili wadudu waharibifu kama vidumuzi wa viazi ” amesema.

Maelezo yake ni kwamba viazi lishe vina kiasi kikubwa cha vitamini A, ambayo ni muhimu kwa watoto chini ya miaka mitano,wamama wajawazito na wanaonyonyesha, pamoja na wazee.
Amesema vitamini A husaidia kuimarisha afya ya macho, pia kwa kinga ya mwili.