Na Lucy Ngowi
DODOMA; NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Athumani Kilundumya ametoa agizo kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kuhakikisha kila kituo kinachowekezwa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kinakuwa na Ofisa kutoka TARI.
Amesema hayo katika Maonesho ya Nanenane ya Kitaifa na Kimataifa yanayoendelea Mkoani Dodoma.
Amesema lengo ni kuhakikisha tafiti zinazofanyika zinatumika moja kwa moja kwa wakulima waliopo maeneo husika.

Amesema uamuzi huo ni sehemu ya mkakati wa serikali wa kubadilisha kilimo kutoka cha kutegemea mvua kuwa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji, kinachotegemea maarifa ya kitaalamu na teknolojia ya kisasa.
“Nataka TARI katika kila kituo tunachowekeza kwa ajili ya umwagiliaji, kuwe na Ofisa wao.
“Hii itahakikisha tafiti zao haziishii makabatini bali zinawafikia wakulima moja kwa moja,” amesema Kilundumya.

Ameongeza kuwa ni lazima tafiti za kilimo ziwafikie wakulima walio vijijini, si tu kwenye makongamano ya wataalamu.
“Tutumie sana tafiti hizi, tusiendelee na kilimo cha mazoea. Tukiwaelimisha wakulima wetu kutumia maarifa haya, tija itaongezeka hata kwa maeneo madogo,” amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhende amesema matumizi ya mbegu bora zilizofanyiwa utafiti ndiyo njia ya kuleta uhakika wa chakula nchini.

“Kinachoweza kufanya uendelevu wa uhakika wa chakula ni matumizi ya mbegu bora zilizofanyiwa utafiti. Tunapongeza kazi nzuri ya TARI, wameleta maboresho makubwa kwenye sekta ya mbegu,” amesema.
Hata hivyo, Dkt. Mhende amesisitiza kuwa ni lazima mbegu hizo ziwe za gharama nafuu ili wakulima wengi waweze kumudu kuzinunua.
“Tusiishie kusema mbegu ni bora. Je, mkulima anapataje hiyo mbegu? Tuwekeze kuhakikisha gharama zinashuka, na mbegu hizo ziweze kuhimili mazingira kwa miaka mingi ijayo,” amesemq.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dkt. Thomas Bwana, alisema kuwa taasisi hiyo imejikita kufanya utafiti wa kina kuanzia afya ya udongo, matumizi ya mbegu bora, hadi hatua za kuongeza thamani ya mazao.
“Lengo letu ni kuongeza tija ya kilimo. Katika msimu huu wa Nanenane, tunatoa elimu hiyo kwenye mabanda yote ya TARI kote nchini,” amesema.