Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MWENYEKITI wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegele, amewataka waandishi wa habari nchini kutumia taaluma yao kuelimisha umma na kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo zOktoba 29, mwaka huu 2025.
Mwambegele amesema hayo leo Agosti mbili. 2025 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kitaifa kati ya Tume na Waandishi wa Habari kuhusu Uchaguzi Mkuu.

Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa vyombo vya habari ni nguzo muhimu ya kuhakikisha uelewa wa wananchi kuhusu mchakato wa uchaguzi unaimarika.
“Taarifa zenu zinaweza kuleta hamasa ya kitaifa au kuzua sintofahamu. Ni wajibu wa kila mwandishi kuhakikisha anawapa Watanzania habari sahihi, kwa wakati na kwa uwiano unaozingatia maadili ya taaluma,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kailima Ramadhani amekumbusha wanahabari kuwa na jukumu la kuhakikisha vyama vya siasa na wagombea wanapata fursa ya kusikika kwa haki katika kipindi cha kampeni.

Ametoa wito kwa vyombo vya habari kuzingatia uwiano wa uwasilishaji wa taarifa, bila upendeleo, ili kuimarisha misingi ya kidemokrasia nchini.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuandika na kuripoti kwa uangalifu mkubwa ili kuepuka kueneza taarifa zisizo sahihi au zinazoweza kusababisha taharuki.
Amesema katika kipindi chote cha uchaguzi, waandishi wanapaswa kutumia majukwaa yao kueneza ujumbe wa amani na mshikamano wa kitaifa.
“Uandishi una nguvu ya kuunganisha au kugawanya. Tunawasihi msitumie taaluma yenu kuwavunja moyo wananchi, bali kuwahamasisha kushiriki kikamilifu, kama wapiga kura au wagombea,” amesema.
Mkutano huu ni sehemu ya mfululizo wa mikutano ya wadau mbalimbali iliyoandaliwa na Tume katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Tangu Julai 27, 2025 Tume imekutana na viongozi wa vyama vya siasa, asasi zisizo za kiserikali, wawakilishi wa wanawake, vijana, watu wenye ulemavu na wahariri wa vyombo vya habari.
Mikutano hiyo itahitimishwa Agosti nne, 2025 kwa kikao maalum na waandaji wa maudhui mtandaoni, pamoja na mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari.