Na Danson Kaijage
DODOMA: BAADHI ya wakazi wa Kata ya Ntyuka, katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wameeleza matarajio yao ya kupata kiongozi mchapa kazi atakayesaidia kusukuma mbele maendeleo ya eneo hilo.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa kikao cha Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Ntyuka, ambapo wagombea nane waliopitishwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa ajili ya kuwania ubunge katika Jimbo la Dodoma Mjini walijitambulisha kwa wajumbe.

Wagombea waliopitishwa ni Samwel Malecela, Rashid Mashaka, Pascal Chinyele, Samwel Kisaro, Fatuma Yusufu Waziri, Robert Mwinje, Rosemeary Jairo na Abdulhabib Mwanyemba.
Baadhi ya wajumbe walieleza kuwa wanatamani kumpata mbunge anayetoka katika maeneo yao na anayezifahamu changamoto za wananchi, wakibainisha kuwa uelewa wa mazingira ya eneo ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya uwakilishi.
Akizungumza mbele ya wajumbe, mmoja wa wagombea, Samwel Malecela, alieleza kuwa iwapo atapata ridhaa ya kupitishwa kwenye kura za maoni, ataweka kipaumbele kwenye kushughulikia changamoto mbalimbali, ikiwemo masuala ya ardhi.
“Jimbo la Dodoma Mjini lina jumla ya kata 21, na kila kata ina changamoto zake. Nia yangu ni kuhakikisha kuwa sauti za wananchi zinasikika bungeni na changamoto zao zinapatiwa majibu kupitia ushirikiano wa pamoja,” amesema Malecela.
Kura za maoni ndani ya chama hicho zinatarajiwa kufanyika hivi karibuni ili kumpata mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao kwa Jimbo la Dodoma Mjini.