Na Mwandishi Wetu
MINSK, BELARUS: KWA mara ya kwanza katika historia ya uhusiano wa kimataifa kati ya Tanzania na Belarus, Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa, amewasili nchini Belarus kwa ziara ya kikazi ya siku nne inayolenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Ziara hiyo ya kihistoria, iliyoanza Julai 21 inatarajiwa kuisha 24, 2025 inaashiria mwanzo mpya wa ushirikiano wa kimkakati katika sekta muhimu zikiwemo kilimo, elimu, afya, utalii, uwekezaji, biashara na teknolojia.

Aidha ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania inayolenga kukuza diplomasia ya uchumi.
Waziri Mkuu Majaliwa alipokelewa kwa heshima kubwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Minsk na mwenyeji wake, Naibu Waziri Mkuu wa Belarus,Viktor Karankevich.
Vile vile wengine waliokuwepo ni Waziri wa Uwekezaji Zanzibar, Sharif Ali Sharif, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Fredrick Kibuta.

Majaliwa anatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi na Waziri Mkuu wa Belarus, Alexander Turchin, ambapo masuala ya ushirikiano wa maendeleo yatapewa kipaumbele.
Pia atashuhudia utiwaji saini wa Hati za Makubaliano zitakazogusa maeneo ya mashauriano ya kisiasa, kilimo, elimu na biashara.
Mbali na vikao vya serikali kwa serikali Majaliwa atakutana na viongozi wa kampuni na taasisi mbalimbali za Belarus kwa lengo la kuvutia wawekezaji kuja Tanzania. Sekta ya kilimo na teknolojia ya viwanda imewekwa kama maeneo ya kipaumbele katika majadiliano hayo.
