Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: RAIS mpya wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mwalimu Suleiman Ikomba, amekuwa kiongozi wa mfano kutokana na historia yake ya kujitoa na kujituma kwa miaka mingi katika kuwahudumia watoto wanaotoka kwenye mazingira magumu.
Ikomba akizungumza na Mfanyakazi Tanzania, ameeleza namna alivyowalea watoto kutoka familia maskini kwa miaka mingi akiwa mwalimu na Mkuu wa Shule katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Wilaya ya Temeke Dar es Salaam.
“Nilikaa na watoto ambao wazazi wao hawakuwa na uwezo nyumbani kwangu kwa wiki sita kabla ya kufanyika Mtihani wa Taifa wa darasa la saba ili niwaandae.
“Wengi wao hawakuwa na mazingira mazuri ya kusoma. Niliwaleta nyumbani, nikatafuta chakula, na nikawasimamia masomo mpaka wakati wa mtihani” amesema Mwalimu Ikomba.
Amesema alianza kazi ya ualimu mwaka 1991, kipindi ambacho ada za shule zilikuwa kikwazo kikubwa kwa watoto wengi kutoka familia za kipato cha chini.
“Nikiwa Mkuu wa Shule, nilikusanya watoto wote waliokuwa hawawezi kulipia ada au mahitaji mengine.
“Nikiwa na mke wangu ambaye pia alikuwa mwalimu, tuliwalea hawa watoto walikula, walisoma na kulala kwetu mpaka tukahakikisha wamefikia malengo yao,” amesema.
Amesema mmoja wa watoto aliowalea kipindi hicho ambaye kwa sasa ameajiriwa, aliungana naye katika kampeni za kuwania urais wa CWT, akionyesha mshikamano na shukrani kwa kile alichofanyiwa na mwalimu huyo huko nyuma.
Amesema katika Shule za Msingi Minazini na Mtoni kwa Mama Mary, Wilaya ya Temeke, Mwalimu Ikomba alianzisha utaratibu wa kup1rishi na wanafunzi wanaotoka katika familia masikini kwa muda wa siku 40 kabla ya mitihani ya kitaifa, kwa lengo la kuwapa fursa ya kujifunza kwa ukaribu zaidi.
“Niliamini kuwa njia ya kweli ya kumkomboa mtoto wa maskini ni kumwezesha kielimu. Hata kama hakuwa na sare, viatu au chakula, nilihakikisha anapata elimu,” amesema.
Amesema katika shule zote alizopita mtu akiulizia kipindi chake kilikuaje, watamuelezea moyo wa kusaidia watoto aliokuwa nao.
Licha ya kujitoa kwake, Mwalimu Ikomba amesema kuna wakati aliumizwa na wazazi kushindwa kuwapeleka watoto shule kutokana na hali ngumu ya maisha.
Amesema hali hiyo ilimvunja moyo kwani hakuweza kuwasaidia watoto ambao hawakufika shuleni.
“Nilikuwa nasubiri watoto wafike, halafu nipambane kuhakikisha wanasoma. Lakini kama hawafiki, nilijisikia kushindwa,” amesema.
Kwa mujibu wa walimu na wazazi waliowahi kushirikiana naye, jina la Mwalimu Ikomba linaenziwa katika maeneo aliyofanyia kazi.
Kwa kuwa Wengi wanamtaja kama kiongozi asiyechoka, aliyewahi hata kushirikiana na taasisi mbalimbali za misaada ili kuhakikisha watoto wa mazingira duni wanapata elimu bora.