Pato la Mwananchi Laongezeka kwa Asilimia 45.4
Na Danson Kaijage
DODOMA: MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Saimon Sirro amesema maboresho makubwa katika sekta ya afya yamechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa ustawi wa wananchi wa Kigoma, hali iliyosababisha kuongezeka kwa pato la mtu mmoja mmoja kwa asilimia 45.4.
Ongezeko hilo ni katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma, Sirro amesema kuwa pato la mwananchi wa Kigoma limepanda kutoka Sh. Mil. 1.4 mwaka 2020 hadi Sh. Milioni 2.1 mwaka 2024.
“Kipato cha wananchi wetu kimeongezeka kwa kiasi kikubwa, na sehemu kubwa ya mafanikio haya yanatokana na uboreshaji wa huduma za afya, upatikanaji wa dawa, na kuimarika kwa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma,” amesema.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, Mkoa wa Kigoma umepokea jumla ya Sh. Bilioni 50.9 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya vituo vya kutolea huduma za afya.

Amesema kiasi hicho cha fedha kimeboresha upatikanaji wa huduma bora za afya katika maeneo ya mijini na vijijini.
“Miundombinu ya afya imeimarika kwa kiwango kikubwa. Hospitali za wilaya zimeongezeka kutoka tatu mwaka 2020 hadi nane mwaka 2025. Vituo vya afya vimeongezeka kutoka 34 hadi 53, na zahanati zimeongezeka kutoka 236 hadi 283,” amesema.
Aidha, upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi umeongezeka kutoka asilimia 86 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 92 mwaka 2025 hatua inayowezesha wananchi kupata matibabu kwa wakati na kuzuia athari za kiafya zinazoweza kuathiri shughuli zao za uzalishaji.
“Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya afya njema na uwezo wa uzalishaji wa mtu mmoja mmoja. Wananchi wetu sasa wanatumia muda mwingi katika kazi na si kwenye foleni za hospitali,” amesema.
Mbali na mafanikio ya sekta ya afya, Sirro amebainisha kuwa hali ya uchumi wa mkoa imeendelea kuimarika, ambapo pato halisi la Mkoa limeongezeka kutoka Sh. Trilioni 4.1 mwaka 2020 hadi Sh. Trilioni 5.6 mwaka 2024 sawa na ukuaji wa asilimia 38.6.
“Kwa ujumla, Mkoa wa Kigoma umepokea zaidi ya Sh.Trilioni 11.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kati ya mwaka 2020 hadi 2025. Fedha hizi zimewekezwa kwenye afya, elimu, miundombinu na sekta nyingine muhimu,” amesema.
Katika upande wa elimu, Sirro amesema kuwa fedha za utekelezaji wa mpango wa elimu bila ada zimeongezeka kutoka Sh. Bilioni 9.60 mwaka 2020 hadi Sh. Bilioni 14.67 mwaka 2025. Idadi ya shule za msingi imeongezeka kutoka 664 hadi 742.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa uwekezaji kwenye afya si tu kwamba unaokoa maisha ya watu, bali pia ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kielimu kwa wananchi wa Kigoma.
“Afya njema ya wananchi wetu ndiyo msingi wa mafanikio haya yote tunayoyaona. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwekeza katika ustawi wa Watanzania, hususan katika maeneo ya pembezoni kama Kigoma,” amesema.