Simiyu Kinara Kitaifa
Na Danson Kaijage – Dodoma
DODOMA: TANZANIA inashika nafasi ya saba duniani kwa uzalishaji wa pamba hai, huku Mkoa wa Simiyu ukitajwa kuwa kinara wa kitaifa katika kilimo hicho chenye tija kwa wakulima.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamlingi Macha amesema hayo alipozungumza na waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dodoma alipokuwa akielezea mafanikio ya serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa sasa zaidi ya asilimia 60 ya pamba yote nchini huzalishwa Simiyu, na uzalishaji umeongezeka kutoka tani 64,594 mwaka 2020 hadi kufikia tani 140,000 mwaka 2024,” amesema.
Amesema Simiyu ndiyo mkoa pekee nchini unaolima pamba hai, ambapo uzalishaji wake umeongezeka kutoka tani 10,300 msimu wa 2021/2022 hadi tani 12,285 msimu wa 2022/2023, nyuma ya mataifa kama China, India, Uturuki na Pakistan.
Amesema hatua hiyo imeiwezesha Tanzania kushika nafasi ya saba duniani katika uzalishaji wa pamba hai.

Amepongeza serikali kwa kufanikisha uboreshaji wa miundombinu ya kilimo, usambazaji wa pembejeo kwa wakati, na uwepo wa wataalamu wa kutosha wa kilimo ambao wamewasaidia wakulima kuongeza tija.
Amesema Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Simiyu (SIMCU 2018 Ltd) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), kimefanikiwa kufufua kiwanda cha kuchakata pamba cha Sola Ginnery kilichopo Wilaya ya Maswa kwa gharama ya Sh. Bilioni 4.0.
“Kiwanda hiki kimeongeza thamani ya pamba kwa wakulima wetu, kimetoa ajira kwa vijana, na pia kimepunguza gharama za usafirishaji wa mazao,” amesema.
Vilevile, Mkoa wa Simiyu umeendelea kuboresha huduma za ugani kwa kuwapatia maofisa ugani vifaa vya kisasa, pamoja na kuwezesha wakulima kwa mikopo midogo ya kilimo kutoka taasisi za kifedha.
“Pamba siyo zao tu, bali ni uti wa mgongo wa uchumi wa wakazi wa Simiyu. Tunaishukuru Serikali kwa kuwezesha mapinduzi haya ya kilimo,” amesena.