Na Lucy Lyatuu
MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umewekeza maeneo salama yenye kuuwezesha kupata faida kubwa ikiwemo hatifungani na dhamana za serikali.
Katika mwaka wa fedha uliomalizika wamepata faida ya sh trilioni 1.3.
Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi PSSSF, Fortunatus Magambo amesema hayo kwenye banda la Mfuko huo katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea kwenye viwanja vya Julius Nyerere,
Amesema asilimia 84 ya uwekezaji uliofanywa na mfuko huo umewekwa maeneo hayo ya hati fungani ambako kuna uhakika yanayouwezesha Mfuko kupata faida kubwa na kulipa wastaafu na wanachama wake mafao mazuri na endelevu.

“Tumewekeza maeneo salama maeneo ambayo yanaleta faida kubwa kwa wakati ili tuweze kulipa mafao bora kwa wastaafu wetu na wanachama, ndiyo maana asilimia 84 ya uwekezaji wetu tumeuwekeza kwenye amana za serikali na hati fungani,” amesema Magambo.
“Tunapokea wafanyakazi wapya kila siku na wengine wanastaafu kwa hiyo wakistaafu wanapaswa wakutane na pensheni yao, ili iwe hivyo lazima tuwekeze fedha zao kwenye maeneo sahihi yenye faida ya haraka na ya uhakika na uwekezaji huu unafuata miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania BoT,” amesema.
Amewahakikishia wanachama wa PSSSF wakiwemo wastaafu kuwa Mfuko uko salama una ukwasi wa kutosha kuhakikisha mafao yanalipwa kwa wakati siku zote.
Alisema PSSSF imekuwa ikijenga nyumba za bei nafuu Tanzania nzima na lengo la kuwa na bei nafuu ni kuhakikisha wanachama wa mfuko huo wanapostaafu kama hawajajenga nyumba wapate nyumba na ambao hawana viwanja wapate viwanja.
“PSSSF tuna ofisi kila mkoa kwa hiyo nawahamasisha wanachama wetu na wastaafu watarajiwa wafike kwenye ofisi zetu waulize nyumba na viwanja waweze kukopa sisi tunataka mstaafu wetu aishi maisha mazuri baada ya utumishi wake ndiyo sababu ya kujenga hizi nyumba za gharama nafuu,” amesema.
Amesema mfuko umewekeza kwenye majengo mengi ya kisasa likiwemo jengo lililopo barabara ya Sam Nujoma lenye orofa 33 ambalo ni bora kwa Afrika Mashariki na Kati kutokana na kujengwa kisasa.
Hata hivyo amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara ambayo yamesababisha jengo hilo refu zaidi kupata wateja kwa asilimia 80.
“Kupata asilimia 80 ya wateja kwenye jengo kubwa kama lile siyo jambo jepesi inamaana kuna kazi kubwa imefanyika na hapa lazima Rais Samia Suluhu Hassan apewe maua yake kwa kuweka mazingira mazuri yaliyovutia wawekezaji kumiminika nchini,” amesema
Amesema PSSSF imekuwa ikijitahidi kujenga majengo yenye ofisi zenye ubora wa kimataifa ili kuwawezesha wawekezaji wanaokuja kuwekeza nchini kupata ofisi zenye hadhi ya kimataifa.
“Maana yetuni kuhakikisha mwekezaji anapokuja hapa apate ofisi ambayo inafanana na ofisi yake ya China au iliyoko Marekani na kwingineko, tunataka apate huduma zile zile ndiyo maana wawekezaji wanazidi kuja nchini kwa kuona ni sehemu salama na sahihi ya kuwekeza,” alisema
Kuhusu eneo la viwanda, PSSSF imeweza kuunga mkono jitihada za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda wamewekeza kwenye viwanda vikubwa viwili ambayo vimeonyesha mafanikio makubwa
Ametaja viwanda hivyo kuwa ni kiwanda cha viatu Karanga International Lather Industry kilichoko mkoani Kilimanjaro ambacho kinatoa viatu bora vinavyouzwa ndani na nje ya nchi.
Magambo alitaja kiwanda kingine kuwa ni cha nyama ambacho kimeongeza ajira kwa watanzania wengi na kuongeza kipato cha wafugaji ambao wamekuwa wakipeleka mifugo yao kuuza kwenye kiwanda hicho.