Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: “BAADA ya kupata mafunzo kwa miaka mitatu nimeweza kukua kibiashara kwa sababu mwanzoni niliweza kuuza bidhaa zangu za viungo vya chakula mkoa mmoja. Lakini sasa nauza nchi nzima hata nje ya nchi,”.
Mnufaika wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi ( SDF), ulioko chini ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Geshoni Muni ameeleza hayo katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba mkoani Dar es Salaam alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania katika Banda la TEA.
Amesema mwanzoni alipoanza usindikaji wa viungo aliuza katika mkoa wa Iringa pekee, lakini sasa anauza mikoa yote bidhaa zake za tangawizi, mdalasini, viungo vya pilau, viungo vya chai na vinginevyo.
“Pia nimebahatika kuuza tangawizi kavu nchi ya Afrika Kusini tani 20 pamoja Zambia.
“Kuwa na TEA kumenisaidia kutambulika na kupata masoko kwa ukubwa kiasi hicho,” amesema.
Ameshukuru kwa kuwa biashara hiyo imemwezesha kuendesha maisha yake, hategemei kuajiriwa wala hawazi kufanya hivyo kwa kuwa anaiamini biashara anayoifanya.
Amekiri maisha yake yameboreshwa kutokana na biashara hiyo.
Naye Mkulima wa Uyoga, Esther Shebe amesema kwamba, naye ni mnufaika wa mfuko huo wa kuendeleza ujuzi.
“Kwa miaka mitatu nimenufaika. Ninashukuru TEA kwa kuniwezesha kunitangaza kwenye maonesho mbalimbali yakiwemo haya ya sabasaba kwa mwaka huu 2025.
“TEA imenipa nafasi ya kuonesha bidhaa zangu na watu wananunua. Lakini nimenufaika kwa kupata ujuzi mpaka nina bidhaa karibia 10 ninazozitengeneza. Lakini hii yote ni kutokana na mfuko wa kuendeleza ujuzi nilipoenda kujifunza SIDO,” amesema.
Amesema kwa sasa anatengeneza losheni ya uyoga, shower jelly pamoja na sabuni ya uyoga na mafuta ya mgando ya uyoga, wine ya uyoga, biskuti, keki na uyoga wenyewe.
Pia ametengeneza mkaa mbadala kwa kutumia mabaki ya uyoga ambao hauna moshi na ni mzuri kwa matumizi.