Na Danson Kaijage
DODOMA: KWA mwaka jana 2024 tani 2,307.37 za bangi zilikamatwa, kati ya hizo tani 2,303.2 zilitoka ndani ya nchi, na 4.17 zilikuwa skansa zilitoka Kusini mwa Afrika.
Hicho kikiwa ni kiasi kikubwa zaidi kilichokamatwa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu William Lukuvi amesema hayo, mara baada kuwasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya kwa mwaka 2024.
Lukuvi amesema, Skanka, ambayo ni bangi yenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC, iliongezeka kwa asilimia 89.8 ikilinganishwa na mwaka juzi 2023, jambo linaloonesha kuimarika kwa udhibiti wa biashara haramu ya dawa hizo kupitia mipaka, viwanja vya ndege na bandari.
Amesema serikali ilikamata tani 1.7 za methamphetamine, kilo 433.02 za heroin, gramu 853 za cocaine, na kwa mara ya kwanza kilo tano za dawa mpya aina ya Methylene-dioxy-pyrovalerone (MDPV).
Zaidi ya hayo ameeleza kuwa tani 18.45 za mirungi, kilo 56.78 za dawa tiba zenye asili ya kulevya na tani 29.6 za kemikali bashirifu zilinaswa kwa usaidizi wa mifumo ya udhibiti wa kielektroniki.
Kwa upande mwingine amesema, Serikali imeendelea kutoa tiba kwa waraibu kupitia vituo 16 vya methadone vilivyohudumia waraibu 17,975,
Pia nyumba 62 za upataji nafuu pia zimeendelea kutoa huduma kwa waraibu 17,230 waliotambuliwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mamlaka hiyo kwa vitendo pamoja na wataalamu wa afya, mashirika ya kiraia, vyombo vya usalama, pamoja na wananchi kwa mshikamano wa pamoja uliosaidia kufanikisha mafanikio hayo.
Amesema, suala la dawa za kulevya si tatizo la sekta moja, linahusisha afya, usalama, elimu, ajira, na ustawi wa jamii,mafanikio ya kweli yanahitaji juhudi jumuishi kutoka serikalini, kwa wananchi, sekta binafsi na wadau wa kimataifa.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, ameonya vikali tabia inayoendelea kushika kasi miongoni mwa wasanii wanaotumia kazi zao kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya.
Amesema, “Tunaendelea kufuatilia kwa karibu nyimbo, video na mavazi yanayochochea utumiaji wa dawa za kulevya, Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa wote wanaopotosha jamii, hasa vijana,”.
Amesena baadhi ya kazi za sanaa zimejaa maudhui ya kashfa, mavazi ya aibu na simulizi za kupambanua matumizi ya bangi na dawa nyingine hatarishi, hali inayochangia kuathiri maadili ya taifa na mapambano ya dawa hizo kwa ujumla.
“Sanaa si jukwaa la kutukuza mihadarati. Vijana wetu wanahitaji maudhui ya kuwajenga, si kuwaangamiza. Tutawachukulia hatua wote wanaokiuka sheria na taratibu za nchi,” amesena.
Amesema Serikali itaendelea kuimarisha mbinu za kiintelijensia, sheria na tiba katika kukabiliana na janga hili la kimataifa, ikiwa ni pamoja na kuhimiza jamii kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapobaini au kushuku shughuli zinazohusiana na dawa za kulevya.