Na Lucy Ngowi
KENYA: WAANDISHI wa Habari Afrika wametakiwa kuandika matatizo wanayokutana nayo wahamiaji wa kazi wa bara hilo wanapokwenda nchi nyingine ili kuyafichua hatua stahiki zichukuliwe.
Rais wa Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ), Omar Faruk Osman amesema hayo wakati wa mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa Chini ya Mpango wa pamoja wa Uhamiaji wa Wafanyakazi (JLMP), kwa ushirikiano na Tume ya Umoja wa Afrika (IOM).

Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika (FAJ).
Osman amesema kwa sababu hiyo, ni vema kutoruhusu habari na historia za Afrika zielezwe na watu wengine kwa namna wanavyotaka wao.
“Hatuwezi kuunda wala kuelezea simulizi ya bara letu au watu wetu ikiwa hatuandiki sisi wenyewe. Mwisho wa siku, uandishi wa habari ni huduma kwa jamii.
“Kama hatuwezi kuwatumikia watu wetu, kama hatuwezi kueleza historia yao kwa namna wanayotaka au inayoakisi uhalisia wao, basi hatufanyi uandishi wa habari kwa ajili ya jamii.
“Tunakuwa kama mashine ya kusambaza taarifa zilizotumwa. Tunachapisha na kukimbiza habari hizo. Lakini historia ya kibinadamu, namna watu wetu wanavyoteseka, namna wanavyodhalilishwa, ni jambo lililo karibu sana nasi—na lazima tufanye jambo kuhusu hilo,” amesema.
Amesema amefurahi kuona kuna ajenda ya vyombo vya habari kuhusu uhamiaji.
“Tunapaswa kutumia fursa hii kueleza historia ya watu wetu, kuonesha mateso ya ndugu zetu wanaorejea wakiwa kwenye majeneza.
“Angalia yanayofanyika katika nchi za Ghuba—ni ya aibu sana. Nchi hizo zinajitajirisha kupitia wafanyakazi wahamiaji. Lakini watu wetu, je, wanatajirika? Hapana. Je, afya zao na ustawi wao vinazingatiwa? Hapana.
“Je, wanakabiliwa na unyanyasaji mkubwa? Ndio. Je, tunasema chochote? Hapana,” amehoji Osman.

Amesema Afrika ina sheria, sera na kanuni nyingi lakini tatizo kubwa lililopo ni utekelezaji wake.
“Wanasiasa wetu, kuanzia wabunge, hawatekelezi kile kinachopaswa kufanyika. Na kwa kuwa hatufanyi hivyo, hatupaswi kuendelea kuzalisha sera mpya kila wakati.
“Tunahitaji kujikita katika kuhakikisha kuwa watu wetu wanalindwa. Na njia pekee ni kufichua madhila hayo.
“Sijui ni wangapi kati yenu mnajua kuwa wiki iliyopita kule Geneva, vyama vya wafanyakazi vya Afrika viliwasilisha malalamiko rasmi dhidi ya Saudi Arabia.
“Ilikuwa malalamiko makubwa na yenye uzito mkubwa zaidi kuwahi kufikishwa kwa ILO dhidi ya nchi hiyo. Watu walidharau—walidhani Waafrika hawawezi kufanya hivyo,” amesema.
Amesema pamoja na kutolewa kwa hoja hiyo vyombo vya habari vya Afrika viliripoti kwa uchache.

“Ukienda uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta kila siku, utaona dada na kaka zetu wakirudi kwa machozi, na si lazima wawe kwenye majeneza.
“Je, tunasimuliaje simulizi hiyo? Ina sura ya kibinadamu yenye kugusa sana. Je, tunawaambiaje Umoja wa Afrika wahakikishe kuwa nchi wanachama wanatekeleza yale waliyoafikiana?
“Je, tunawafichuaje wanasiasa wala rushwa wanaoshirikiana na Waarabu matajiri wanaofadhili serikali zetu ili kuficha madhila haya? Je, tunainuaje hadhi ya Waafrika? Je, tunasemaje kuwa “maisha ya watu weusi ni muhimu” kwa njia yetu sisi wenyewe? Hili ni muhimu sana,” amehoji.
Amesema waandishi wa habari wanapaswa kuzungumza kwa niaba ya waafrika, kuwapa sauti, kueleza historia yao na kuifichua wanayotendewa.