Na Danson Kaijage
DODOMA: NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema serikali imetoa ruzuku ya asilimia 20 hadi 50 kwenye mitungi ya gesi ya LPG 452,445 kwa watumiaji wa mwisho ikiwa ni jjtihada za kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Kapinga ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Grace Tendega aliyetaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa muda mfupi wa kuhakikisha Wananchi wa Vijijini wanatumia Nishati Safi ya kupikia badala ya Kuni na Mkaa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti Serikali kupitia REA pia itasambaza majiko banifu 200,000 yenye bei ya punguzo la hadi asilimia 75 pamoja na kuwezesha ufungaji wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi za Umma zinazohudumia watu zaidi ya 100,” amesema.
Vile vile amesema Serikali imekamilisha kazi ya usambazaji umeme katika vijiji vyote hivyo kwa sasa inaendelea kuhimiza matumizi ya majiko ya kupikia yanayotumia umeme ikiwa ni njia mojawapo ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wa vijijini badala ya kutumia kuni na mkaa.
Amesema Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia ni wa miaka 10 lakini serikali inao mkakati wa matumizi bora ya nishati ambao unahusisha pia sekta binafsi kwa ajili ya kusaidia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Akijibu swali la Mbunge wa Mbulu, Zacharia Isaay aliyeuliza Serikali imejipangaje kuhakikisha Vitongoji vyote vilivyokusudiwa katika mwaka huu wa bajeti kufikiwa na umeme katika kipindi cha mwezi mmoja uliobaki, Kapinga amesema Serikali inayo mikakati na miradi mbalimbali ya kupeleka umeme katika Vitongoji.
Amesema kuwa, moja ya mikakati hiyo ni kupeleka umeme katika Vitongoji 15 kwa kila Jimbo, na pia Serikali ina mkakati wa kupeleka umeme katika Vitongoji 20,000 ambapo awamu ya kwanza inaanza kupeleka umeme katika Vitongoji 9000 na hatua iliyopo ni utafutajj wa wakandarasi.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Anatropia Theonest aliyeuliza bei ya Serikali ya ruzuku imeanza kutumika lini kutokana na mitungi ya gesi kuendelea kuuzwa kati ya Sh. 22,000 na 25,000 na kwa mitungi mikubwa ya kilo 15 Sh. 50,000 na 60,000.
Amesema maeneo ya mjini Serikali imepeleka ruzuku hadi asilimia 25 na maeneo ya Vijijini ni kati ya asilimia 50 hadi 75 na kutolea mfano iwapo mtungi ulikuwa unauzwa Sh. 45,000 kwa bei ya ruzuku inapatikana kwa Sh. 17,000 hadi 21,000 na kusema ni zaidi ya nusu ya bei yake.
Amesema katika kila Wilaya kuna takribani mitungi 3,255 inayopatikana kwa ruzuku na kuongeza kuwa ndio kwanza mkakati umeanza.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Yustina Rahhi aliyeuliza mpango wa Serikali kuwapelekea jamii ya wafugaji teknolojia ya biogas au kuwajengea majiko yanayotumia samadi ya gesi ambayo ni rahisi, Kapinga amesema Serikali inatekeleza mradi huo kupitia umoja wa Ulaya (mfuko wa UNCDF) ambao una teknolojia alizozitaja Mbunge.
Akijibu swali la Mbunge wa Nyang’wale, Hussein Amar aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali kuzipelekea nishati safi ya kupikia Shule za Sekondari 19 na Sekondari 12 za bweni zilizo Wilaya ya Nyang’wale ili kulinda mazingira, Kapinga amesema Wizara ya Nishati inaompango wa kuzipelekea nishati safi ya kupikia Taasisi za umma kwa kushirikiana na TAMISEMI.
Katika hatua nyingine Kapinga amezishauri Halmashauri kufunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Taasisi zilizopo katika Halmashauri wanazoziongoza kwa kutumia mapato ya ndani.