Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WADAU 436 wa tasnia ya maziwa nchini wamesajiliwa kati ya 800 waliolengwa ambao ni sawa na asilimia 54.5.

Mwakilishi wa Msajili Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Deorinidei Mng’ong’o amesema hayo katika semina iliyoandaliwa na bodi hiyo kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) katika kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Duniani.
Kilele cha maadhimisho hayo ni Juni mosi, mwaka huu mkoani Morogoro. Malengo yake ni kuhamasisha matumizi ya maziwa, pia matumizi ya maziwa salama.
Amesema bodi hiyo imefanikiwa kusajili wazalishaji 130, wasindikaji 69, wafanyabiashara 86. Waingizaji maziwa nchini 24, wauzaji maziwa nje ya nchi 10, wasambazaji wa maziwa saba, na wakusanyaji maziwa 41.

Pia amesema bodi hiyo imewezesha kusajiliwa kwa maghala 33 ya kuhifadhia maziwa sambamba na wauzaji wa pembejeo watatu, wachuuzi wa maziwa tisa, na wasafirishaji wa maziwa 24.
Amesema pia wameweza kurasimisha biashara ya maziwa na kupunguza uuzaji holela.
Vile vile TDB imewezesha uanzishwaji wa sehemu naalum ya kuuzia maziwa mbili katika maeneo ya Kisasa Sekondari na Uhindini jijini Dodoma.
Ameelezea mafanikio mengine ni pamoja na kuweka mashine mbili za kuuzia maziwa eneo la Uhindini Dodoma, na Njiro jijini Arusha.

Kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na bodi hiyo, uzalishaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita bilioni 3,969,887,235.76 mwaka 2023/ 2024 hadi lita 4,009,985,321.22 mwaka 2024/ 2025 sawa na ongezeko la asilimia moja.
Kati ya lita hizo lita 2,605, 008,464 zimetokana na ng’ ombe wa asili, lita bilioni1,404,976,867 zimetokana na ng’ombe wa maziwa walioboreshwa
“Ongezeko la uzalishaji wa maziwa limechangiwa na utoaji wa elimu ya ufugaji bora na wa kibiashara, na kuongezeka kwa ng’ombe bora wa maziwa walioboreshwa,” amesema.

Mafanikio mengine amesema ni kuongezeka kwa vituo vya kukusanya maziwa kutoka 258 mwaka 2023/ 2024 hadi 269 mwaka 2024/ 2025, kufanya ukusanyaji wa maziwa kuongezeka kutoka lita 93,427,734.54 mwaka 2023/2024 hadi lita 95,614,978.76 mwaka 2024/ 2025 sawa na ongezeko la asilimia 2.4.
” Aidha usindikaji wa maziwa umeongezeka kutoka lita 81,800,654.8 mwaka 2023/ 2024 hadi lita 90,416,788.5 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 11.7.
” TDB inaendelea na utekelezaji wa program ya utoaji elimu na unywaji wa maziwa shuleni katika shule 149 nchini.
“Na jumla ya wanafunzi 102, 446 wanashiriki katika mpango hadi Machi , 2025,” amesema.
Amesema nakala 3,600 za Mpango wa unywaji maziwa shuleni kuanzia mwaka 2023 hadi 2028 zimesambazwa, inatarajiwa kuwa wanafunzi 1,609,687 watafikiwa kupitia program hiyo ifikapo mwaka 2027/ 2028.
Bodi hiyo ni taasisi ya serikali inapspimamia, inatatibu na kuendeleza tasnia ya maziwa nchini.