Na Danson Kaijage.
DODOMA: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema Serikali inatambua, inathamini michango mikubwa ya wabunifu na itaendelea kuwaenzi akiwemo Mzee Morrissi na ngoma zake 10.
Profesa Kabudi amesema hayo Jijini Dodoma katika Ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.
Amesema utakapomalizika ujenzi mkubwa wa Shirika la Utangazaji TBC kutakuwa na sehemu muhimu ya makumbusho ambayo yataonyesha kazi zilizofanywa na wabunifu hao pamoja na ngoma 10 za mzee Morris.
Pia amesema katika kupiga ngoma zake ambazo husikiwa na shirika la utangazaji la TBC wakati wa kutangaza saa au taarifa ya habari ni sehemu muhimu ya kumuenzi.
Kabudi amesema Tanzania ndiyo nchi pekee yenye anuai kubwa ya Utamaduni na lugha Barani Afrika.
Amesema kwa upande wa Lugha Tanzania ndiyo yenye makundi yote ya lugha mengi kuliko nchi yoyote Afrika.
“Tuna makundi ya lugha ya kibantu ukichukua Afrika ya Magharibi wote ni wa bantu, tunaweza kuwa na makabila 600 lakini wote ni wabantu.
“Lakini sisi tuna makabila ambayo asili yao ni kibantu,wengine ni Waniloti na Waniloti ni makundi mawili kwenye Mbuga yani Wamasai na wale wa kwenye mito Wajaruo.
“Lakini pia sisi tunao Wakoisani wapo Kondoa,Ovada mpaka Manyoni,lakini sisi pia tunawatu wanaozungumza lugha za Kiafloatiki ni Wairaq na Wamburu,” amesema.
Ameeleza Tanzania ndiyo nchi ambayo ina mshikamano na umoja mkubwa kuliko nchi yoyote Barani Afrika Kusini mwa Sahara kwa sababu Tanzania sasa ni Taifa siyo mkusanyiko wa makabila na Rais Samia Suluhu Hassan aliendeleza hilo.
“Lakini pamoja na umoja huo tunaouona bado sisi ndiyo wenye anuai kubwa ya Utamaduni na lugha ambazo hazifanani lakini tumewekwa pamoja kama Taifa,” amesema.