Na Mwandishi wetu
DAR ES SALAAM: KITUO cha Sheria Na Haki Za Binadamu (LHRC), kimeahidi kufanyakazi na Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari (JOWUTA) katika kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu sheria za kazi na sheria zinazohusu sekta ya habari.
Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho LHRC, Fulgence Massawe ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na viongozi wa JOWUTA Makao Makuu ya LHRC.
Massawe amesema LHRC ni mdau mkubwa wa wanahabari na tasnia ya habari hivyo wakati wote wapo tayari kufanyakazi na JOWUTA kusaidia kuboresha tasnia ya habari nchini.

“Tunajua changamoto katika sekta ya habari,i kiwepo asilimia zaidi ya 80 ya wanahabari kutokuwa na mikataba wala ajira lakini pia tunajua uchumi mbaya wa vyombo vya habari,” amesema
Amesema uchumi mbaya wa vyombo vya habari sio kigezo cha kushindwa kuheshimiwa sheria za kazi zilizopo nchini.
“Tutashirikiana kutoa elimu kwa wanahabari,waajiri na wadau ili kuona ni jinsi gani waandishi wanafanyakazi kwa kuzingatia maadili lakini wanakuwa na uhuru wa kufanyakazi na katika mazingira bora,” amesema.
Mwenyekiti wa Taifa wa JOWUTA Mussa Juma amemweleza Massawe kwamba, JOWUTA inahitaji ushirikiano na wadau mbalimbali katika kutetea maslahi bora ya waandishi wa habari.
“Bado kuna waajiri wengi hawalipi wanahabari na wala hawatoi mikataba jambo ambalo ni kinyume cha sheria za kazi hivyo JOWUTA itaendelea kupigania haki za wanahabari ikiwepo mazingira bora ya kazi,” amesema.
Amesema tayari JOWUTA imesaidia baadhi ya wanahabari kwenda mahakamani kudai stahiki zao lakini bado changamoto ni kubwa.
“Tumekuja hapa kujadiliana juu ya ushirikiano wetu lakini pia kama viongozi wapya wa JOWUTA kujitambulisha kwa wadau,” amesema.
Juma ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji wa Shirikisho la Waandishi wa Habari Afrika Mashariki na Kati, ametaka LHRC kufanya kazi na JOWUTA hasa kuelekea katika chaguzi ambapo wanahabari wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi.
Naye Katibu Mkuu wa JOWUTA Seleman Msuya amesema JOWUTA ndio chama pekee kisheria nchini chenye jukumu la kulinda na kutetea maslahi bora ya kazi kwa waandishi na mazingira bora ya kazi.
“Sisi ndio tunaweza kuwapeleka waajiri mahakamani na tunafanya hivyo lakini bado changamoto ni nyingi ndio sababu tunaomba ushirikiano na wadau wakiwepo LHRC,”amesema.
Katika ziara hiyo pia mweka hazina wa JOWUTA Lucy Ngowi amesema kutokana na hali ngumu za kimaisha kwa waandishi wengi hata uchangiaji wa ada za chama imekuwa ni tatizo.
Viongozi wa JOWUTA bado wanaendelea na ziara kwa wadau mbalimbali kuelekea uzinduzi wa mafunzo ya wanahabari kuhusiana na kuripoti vyema uchaguzi mkuu lakini wakiwa salama ikiwepo kutonyanyaswa na vyombo vya dola ama vyama vya siasa.
.