Na Shani Kibwasali
SINGIDA: RAIS wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania ( TUCTA), Tumaini Nyamhokya amesema
Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi kitaifa kwa mwaka 2025 ijulikanayo kama Mei Mosi yatafanyika mkoani Singida.
Nyamhokya amesema hayo katika kikao cha maandalizi ya maadhimisho hayo na kamati ya maandalizi kuangalia namna sherehe hiyo itakavyofanyika.
⁹
Amesema, ” TUCTA imefurahishwa kwa namna maandalizi yalivyoanza ikiwa pamoja na kupokelewa vizuri na Mkuu wa Mkoa Halima Dendego pamoja na Katibu Tawala wake hivyo ni ishara tosha kabisa mambo yatakuwa sawa,”.
Amesema viongozi wa TUCTA wamejipanga na wako tayari kushirikiana na viongozi wa Mkoa wa Singida kufanikisha sherehe hiyo.
“Ninaamini itakuwa ni Mei Mosi ya Kipekee itakayofanyika. Tuko tayari muda wowote na vikao vyote vitakavyokuwa vinapangwa tutakuwa tayari,
“Na majuma mawili ya mwisho viongozi wa shirikisho tutaweka timu hapa kuhakikisha jambo hili linafanyika kwa ufanisi,” amesema.
Amesisitiza kuwa,”Singida ipo tayari kuwapokea wageni wote wataishi vizuri, wenye hofu ya malazi watalala vizuri, kila kitu kipo sawasawa,”.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dendego amesema watakuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2025.
Amesema maadhimisho hayo yatafanyika kwenye Uwanja wa Liti uliopo Manispaa ya Singida.
Ameongeza kuwa, sherehe hizo zitatanguliwa na michezo mbalimbali, pia utafanyika utalii wa ndani ya mkoa ili kuonyesha wageni watakaofika mambo mbalimbali, ikiwemo fursa za Kiuchumi na kiuwekezaji.
” Maadhimisho hayo yatapambwa na mambo mbalimbali, na kabla ya kilele kutakuwa na usiku wa Kuku ‘ Kuku Festival’,
” Mashindano ya Magari, Mashindano ya Ngumi, Maonesho Mbalimbali na shughuli zinazofanywa na Wana Singida,” amesema.
Ameeleza pia kutakuwa na burudani mbalimbali zikiwemo ngoma za asili, pamoja na wasanii wakubwa nchini.