Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAFANYAKAZI kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), wametembelea kiwanda cha COTWORLD, kujifunza kuhusu teknolojia mpya ya ujenzi wa nyumba za kisasa bila kutumia tofali.
Wafanyakazi hao ni kutoka VETA Makao Makuu na Kanda ya Dar es Salaam, waliongozana na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore katika kiwanda hicho kilichopo Kigamboni.

Mkurugenzi Mkuu huyo Kasore amesema, lengo la kutembelea kiwanda hicho ni kuangalia namna VETA na COTWORLD wanavyoweza kushirikiana ili kuwezesha wanafunzi wa vyuo vya VETA kupata mafunzo ya vitendo kuhusu teknolojia hiyo.
Amesema teknolojia hiyo inahusisha matumizi ya chuma katika kusimamisha kuta badala ya tofali, mbinu inayolenga kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika sekta ya ujenzi.

Amesema VETA inaendelea kuimarisha ushirikiano na viwanda ili kuhakikisha wanafunzi wake wanapata ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Tunahitaji kuwapa wanafunzi wetu maarifa na ujuzi wa kisasa ili waweze kushindana katika sekta ya ujenzi inayobadilika kwa kasi. Ushirikiano na viwanda kama COTWORLD ni hatua muhimu katika kufanikisha hili,” amesema.
Katika ziara hiyo, viongozi wa VETA walitembelea sehemu mbalimbali za kiwanda hicho na kushuhudia mchakato wa uzalishaji wa vifaa vya ujenzi vinavyotumika katika teknolojia hiyo mpya na kubaini fursa za mafunzo kwa wanafunzi wa VETA.

Baada ya ziara hiyo, pande zote mbili zimeahidi kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa vitendo katika ujenzi wa nyumba za kisasa.
