Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: HATIMAYE Biashara ya saa 24 kuanza leo katika eneo la Kariakoo, Mkoa wa Dar es Salaam.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza hayo jana usiku akiwa katika maeneo ya Kariakoo.
Amesema kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo hadi Februari 27, 2025 unafanyika uhamasishaji kwa umma kuhusu uanzaji rasmi wa ufanyaji biashara kwa saa 24.
Amesema Kariakoo ni eneo la uzinduzi lakini wilaya nazo zitaendelea kufanya hivyo Katika maeneo yao ili kuweza kurasimisha biashara saa 24.
Chalamila amesema Mataifa yaliyoendelea hufanya biashara saa 24 ambayo hupanua wigo wa ajira kwa vijana, lakini pia kodi huongezeka.
“Kwa kuwa Mkoa huu ni kitovu cha Biashara kwa kufanya hivyo vijana watapata fursa za kujiajiri na TRA pia itaweza kukusanya mapato mengi zaidi,” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa, amewahakikishia wafanyabiashara usalama wa kutosha kwa kuwa miundombinu ya kiusalama inaendelea kuimarishwa ikiwemo kuwekwa taa na Camera katika Mitaa.
Pia amesema baada ya uzinduzi huo anatarajia kuunda kamati itakayoongozwa na Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Toba Nguvila kwa ajili ya kupitia sheria zinazokinzana na kufanya biashara saa 24 hasa Sheria ndogo ndogo za Halmashauri za Manispaa.