Na Lucy Lyatuu
TANZANIA itakuwa mwenyeji wa mkutano na maonesho ya 11 ya Petroli ya Afrika Mashariki (11TH East African Petroleum Conference and Exhibition – EAPCE’25), unaotarajiwa kufanyika Machi 5 hadi 7, 2025 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam.
Kauli mbiu ya Mkutano huo, ni “Kufungua Fursa za Uwekezaji katika Nishati, Mchango wa Rasilimali za Mafuta katika Kupata Nishati ya Uhakika kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika Mashariki,”.
Mkutano huo utafunguliwa rasmi na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ukitanguliwa na semina kuhusu masuala ya nishati safi ikiwemo nishati safi ya kupikia na matumizi ya gesi kwenye magari (CNG) itakayofanyika Machi 4, 2025.
Mkutano wa EAPCE’25 utawaleta pamoja washiriki zaidi ya 1000, wakiwemo watunga sera, viongozi wa Serikali kutoka nchi mbalimbali ikiwemo nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wawekezaji wa kimataifa na wa ndani.
Akizungumza na vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba amesema Mkutano huo utatoa nafasi ya kujadili mchango wa rasilimali za mafuta na gesi asilia katika mchanganyiko wa nishati kwa maendeleo endelevu ya Afrika Mashariki.
Pia washiriki watajadili fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi Afrika Mashariki.
Aidha, Mramba ameeleza kuwa mada mbalimbali kutoka kwa wataalam na wabobezi katika sekta ya mafuta na gesi zitatolewa zikiwemo utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi katika nchi za Afrika Mashariki.
Amesema mada nyingine ni fursa za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi, dhana ya kuelekea nishati safi, masuala ya mazingira, miundo ya kisera, kisheria na kiudhibiti katika mafuta na gesi na kadhalika.
Vilevile, mkutano utahusisha maonesho ya bidhaa na huduma kutoka kampuni mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi asilia.
Aidha,Mramba ameeleza kuwa Mkutano wa EAPCE’25 unafanyika katika wakati muhimu baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kujadilia masuala ya nishati.
Katika mkutano wa Mission 300 nchi za Afrika zilikubaliana kuweka Mpango Mahususi wa Taifa wa Nishati kwa kipindi cha miaka mitano 2025-2030.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kikanda ya maandalizi ya EAPCE’25 ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio aliongeza kuwa Mkutano huu unahusisha pia ziara za kitaaluma katika maeneo ya kijiolojia katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuwapa washiriki mtazamo wa vitendo kuhusu sekta.