Na Mwandishi Wetu
SHULE tatu zilizonufaika na miradi ya Mfuko wa Elimu wa Taifa baada ya kukamilika kwa ujenzi wake katika Halmashauri za Wilaya ya Mtama mkoani Lindi na Masasi (Mtwara), zimekabidhiwa vyeti.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Dkt. Leonard Akwilapo amekabidhi vyeti hivyo kama ishara ya kuwakabidhi rasmi miradi hiyo kwa ajili ya matumizi na usimamizi.
Dkt. Akwilapo amekabidhi vyeti hivyo
wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye halmashauri hizo. Pia amekagua maendeleo ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na TEA kwa ufadhili wa Mfuko wa Elimu wa Taifa.

Akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Masasi, James Chitumbe, Dkt. Akwilapo amesema ameridhishwa na ubora wa miradi iliyokamilika.
“Katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, nitakabidhi cheti kwa ajili ya mradi wa nyumba nne za walimu katika Shule ya Sekondari Lupaso, ambayo pia ina mradi mwingine wa jengo la utawala ambalo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 80,” amesema.

Vile vile katika Wilaya ya Mtama, amekabidhi vyeti kwa miradi ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Songambele na bweni moja la wanafunzi lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika Shule ya Sekondari Mnara, ambalo limekamilika kwa asilimia 100.
Kwa niaba ya wanufaika wa miradi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Chitumbe, ameishukuru TEA kwa kufadhili miradi hiyo, akisema imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya elimu katika shule husika.
Mbali na kukabidhi miradi hiyo iliyokamilika, Dkt. Akwilapo pia alitembelea miradi mingine inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo ujenzi wa maabara ya sayansi na nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari Ngongo iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Lindi.