Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: BARAZA la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC), limetoa rai kwa Jeshi la Polisi Usalama Barabarani na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), kutilia mkazo ufuatiliaji wa usalama wa vyombo vya usafiri kuelekea mwisho wa mwaka.
Aidha ufuatiliaji wa sheria za usalama barabarani kwa madereva wawapo safarini.
Katibu Mtendaji wa baraza hilo, Daud Daudi ametoa rai hiyo alipozungumza na Waandishi wa Habari akielezea usafiri wa ardhini kuelekea. Wisho wa mwaka 2024.
Daudi amezitaka mamlaka hizo pia kufanya uhakiki endelevu wa vigezo vya vyombo ikiwemo bima na kuhakiki huduma itolewayo kama inalingana na madaraja. Yaliyochaguliwa na abiria.
“Kuhakikisha hakuna muda ambao unajulikana kama ‘wasimamia sheria hawapo’ hasa nyakati za usiku ili kuhakikisha usalama wajati wote kwa abiria wawapo safarini,” amesema.
Vile vile amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara yatokanayo na ajali zinazoepukika.
Ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vyombo vya usalama vyenye hitilafu havitumiki kutoa huduma za usafiri kwa kuhakikisha ukaguzi unafanyika kwa weledi.
Kwa upande wa abiria amewataka kutoa ushirikiano kwa watoa huduma ili kuwawezesha kupatiwa huduma zenye viwango vizuri.
Amesisitiza kuwa mapumziko ya mwisho wa mwaka kwa miaka mingi yamekuwa yakiambatana na uhitaji mkubwa wa wasafiri kuelekea sehemu mbalimbali za nchi.