Na Lucy Ngowi
PWANI: “SASA mtakwenda kupika chakula kwa haraka na kwa usafi na hii itasaidia katika shughuli zenu kwa pamoja tutamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambayo italinda afya zenu pia,”.
Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni mbunge wa Chalinze amesema hayo wakati wa ugawaji wa majiko ya gesi 118 kwa mamalishe 15.

Ridhiwani amesema lengo kubwa la kugawa majiko hayo ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kutunza mazingira na kuwafanya wananchi kuondokana na matumizi ya nishati chafu.
Naye Ofisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa dawati la Jinsia, Halmashauri ya Chalinze, Recho Mnguruta amesema majiko hayo yatakwenda kuwasaidia wanawake wajasiriamali kuondokana na kutumia kuni na mkaa.

Mkazi Lwa Msata Lilian Skawa amemshukuru Mbunge wa Jimbo hilo Ridhiwani kwa kuwapatia majiko hayo ambayo yatawarahisishia kwenye kazi yao kupika kwa haraka na kuwapatia wateja wao chakula cha moto muda wote.
Amesema kipindi cha mvua walikabiliana na changamoto ya mkaa kutokana na kupatikana kwa shida, hivyo kwa sasa wanakwenda kuwa na mabadiliko ya kupika kwa wakati chakula na kwa hali ya Usafi.