Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amesema Tanzania ipo tayari kuanza majadiliano kuhusu urejeshwaji wa mikusanyo ya malikale na masalia ya miili ya binadamu iliyochukuliwa na Ujerumani wakati wa ukoloni
Chana aliyasema hayo kwenye Uzinduzi wa Onesho la pamoja kati ya Tanzania na Ujerumani kuhusu Historia za Tanzania lililowekwa katika Jumba la Humboldt mjini Berlin, Ujerumani
Akiongea kwa njia ya mtandao amesema Kamati ya Majadiliano tayari imeundwa na mawasiliano yanaendelea kwa upande wa Ujerumani kupitia njia za kidiplomasia.
“Kuwekwa kwa Onesho hili la pamoja pia ni ishara nzuri ya kwamba Serikali ya Ujerumani ipo tayari kurejesha heshima ya utamaduni wa Mtanzania na kuweka alama ya uwajibikaji wa kudumu na uwajibikaji wa kimaadili kwa historia ya ukoloni iliyotweza utu na ustawi wa Mtanzania” alisema Chana.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Utamaduni na Habari wa Ujerumani, Claudia Roth, Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Hassan Iddi Mwamweta, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Taifa, Dr. Noel Lwoga, Mkurugenzi Mkuu wa Humboldt Forum Profesa Hartmut Deorgerloh, na baadhi ya Machifu na wanajamii kutoka Tanzania. baadhi ya machifu na wanajamii kutoka Tanzania.