Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema kwa mara ya kwanza serikali inapeleka wauguzi 101 nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kwenda kufanya kazi huko.
Ridhiwani amesema hayo leo Novemba 28, 2024 katika hafla ya kuwaaga watanzania wanaoenda kufanya kazi nchini Saudi Arabia.
“Tukio hili ni la kipekee sana, kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kupeleka watanzania wataalam kwenda kufanya kazi nje ya nchi kwa utaratibu rasmi unaoratibiwa na serikali.

“Aidha ni la kipekee kwa kuwa ni matunda ya kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwezesha watanzania kunufaika na diplomasia ya kiuchumi,” amesema.
Amesema kupelekwa kwa wauguzi hao ni matokeo ya kusainiwa kwa hati mbili za ushirikiano kati ya Tanzania na Saudi Arabia Novemba mwaka jana kuhusu uratibu wa ajira za watanzania nchini Saudi Arabia.
“Watanzania hawa tunaowaaga ni sehemu tu ya watanzania wengi watakaokwenda kufanya kazi nchini Saudi Arabia,” amesema.
Ridhiwani amesema suala la kuwezesha watanzania kunufaika na fursa za ajira nje ya nchi ni moja ya vipaumbele vya serikali katika kuongeza fursa za ajira kutoka watanzania 556,065 mwaka 2022 hadi milioni moja ifikapo 2028.
Pia kuongeza fedha zinazohamishwa na watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi kutoka dola za kimarekani milioni 697.9 mwaka 2022 hadi bilioni 1.5 mwaka 2028.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mohamed Juma Abdalah amewakaribisha wauguzi hao, pia amewataka kulinda maadili na utamaduni wa kitanzania.
Pia amewataka kuzingatia taratibu, sheria na kanuni za nchi husika.